Ruka hadi kwenye maudhui makuu

RIWAYA: JERAHA LA HISIA SEHEMU YA TATU

MTEULE THE BEST

Uwanja Wa Simulizi's photo.

RIWAYA: JERAHA LA HISIA
MTUNZI: George Iron Mosenya
Mawasiliano: 0655 727325
SEHEMU YA TATU
Naomi hakuwa na pombe kichwani, akili zilikuwa timamu kabisa,alikuwa anatetemeka sio kwa baridi bali uoga mkubwa sana,alikuwa amekodoa macho macho yake, akili ilimruhusu kwenda mbele lakini miguu ikiwa mizito kama amevaa viatu vya chuma.Jasho likamtoka licha ya mvua iliyokuwa imenyesha.
* * * *
Jeuri ya pesa aliyokuwa nayo ilimpelekea Dj Walter kufanya manunuzi ya bei ghali sana kwa fujo, alikuwa na furaha kubwa sana kurejea Tanzania kushehereke sikukuu za mwisho wa mwaka pamoja na familia yake. Lakini furaha yake kubwa ilikuwa maendeleo mazuri kiafya ya dada yake Maureen.
Gari yake mpya aina ya Land Cruiser Prado ilikuwa imechafuka kwa mapochopocho. Malipo mazuri aliyokuwa akilipwa yalimfanya Walter awe mmoja kati ya watu maarufu na wenye fedha nchini Uganda lakini hakulewa sifa aliendelea kuwa karibu na Anko Muga na sasa walikuwa naye ndani ya gari wakisafiri kwenda Tanzania. Walter alikuwa yupo kwenye usukani akipambanisha tairi za gari na ardhi kuelekea Tanzania.
Ilikuwa safari ndefu lakini yenye uhakika kutokana na ubora wa gari. Majira ya saa tano usiku mvua kali iliwapokea jijini Dar-es-salaam, Muga alishauri waende hivyohivyo hadi Tabata Aroma lakini Walter hakuafiki kutokana na uwepo wa bonde kubwa jirani na nyumba ya Frank ambalo hujaa maji na kuzuia magari kupita vyema. Walter alihofia kunasa na kushindwa kuifikisha ‘surprise’ nyumbani kwa Frank.
Royal in Hotel ndipo walipoamua kupumzika hadi asubuhi,Walter alikuwa wa kwanza kuamka kisha Muga. Wakati akiwa maliwatoni ndipo Muga naye alipoamka, wakajiandaa kwa hatua kisha wakaondoka kwa pamoja.
Majira ya saa nne asubuhi tayari kupitia kioo kikubwa cha mbele Walter aliweza kuiona nyumba ya Frank, nyumba ambayo ndani yake alikuwepo dada yake mpenzi aitwaye Maureen, Walter alitamani kupaa na kujikuta ndani ili amkumbatie dada yake lakini hakuwa na namna ilikuwa lazima avute subira.
Umati mkubwa uliokuwa eneo lile ulimshangaza kwa kiasi fulani, alidhani huenda amekosea njia ya kupita ama la akaiwazia ile mvua kuwa huenda iliezua paa la nyumba ya jirani yeyote. Yote haya yalipita kama upepo kwa kasi ya ajabu. Muga yeye alikuwa kimya, akisikiliza muziki kupitia simu yake.
"Mh! wamejuaje ninakuja? au...bamdogo Frank ameoa...au ni birthday ya..." alijiuliza yote hayo Walter lakini Muga hakuwa na jibu lolote. Aliendelea kutikisa kichwa kuashiria anavyoburudika na muziki.
"Harusi gani kelele hivi?" aliendelea kuuliza Dj safari hii akiwa kama anayezungumza mwenyewe, huku akishuka kwenye gari bila kuzimisha injini, nyuma yake alifuata Muga.
Kwa mbali akahisi hofu. Huu umati ulimkumbusha miaka kadhaa nyuma, lilikuwa eneo hili hili analolitazama kwa wakati huu, umati mkubwa ulijaa, majeneza matatu yakapangwa kwa ajili ya kuaga miili ya marehemu baba na mama yake pamoja na bibi yake kipenzi waliozoeana sana.
Walter akafadhaika moyoni, miguu ikawa mizito. Alipoyafumba macho yake alikumbuka kuwa siku ya msiba ule usiofutika akilini mwake kulikuwa na vilio vikuu, lakini leo hapa kuna kelele tupu na watu hawana utulivu.
Kuna nini? Alijiuliza kijana huyu ambaye alikuwa na kila hadhi ya kuitwa mtanashati.
Jibu angelipata kwa kulifikia eneo la tukio.
****
Tumbo lililoanza ghafla kumuuma Maureen lilipelekea msichana huyu anayehitaji uangalizi wa karibu sana, kwa kujikaza na kujivuta vuta hadi akaufikia mlango wa sebuleni, alifanya hivi kwa kuwa alikosa msaada, kama ni kulitaja jina la Naomi alilitaja kwa kurudiarudia lakini bado hali ilikuwa ileile. Akaifikia sebule ambapo alipokelewa na mvua kali ya upepo, maumivu yalivyozidi huku akiwa pale mlango Maureen akiwa na nguo yake laini ya kulalia alimaliza haja zake palepale, lakini bado tumbo liliendelea kuuma, mvua nayo ilikuwa inanyesha bado,taratibu alijaribu kupapasa wapi pa kupita arejee chumbani lakini giza likamsaliti na uwezo mdogo wa kuchanganua mambo baada ya kuwa amepata utindio wa ubongo, akajikuta amepotea njia katika hali ya kusikitisha tena iliyomtia katika mateso makuu. Maureen aliishia kulivagaa kabati la vyombo, vikatelemka baadhi vikamponda kichwani, akatokwa na yowe la hofu, mara akahamia katika luninga, nayo akaanguka nayo huku redio ikimponda vidole, akalia tena kwa uchungu mkubwa. Katika kujikwamua kutoka katika redio iliyobana kidole chake Maureen ambaye yu gizani akajikuta akiangukia mbali kwa maumivu makali akajikunja hadi akasalimiana na sakafu iliyokuwa inazidi kuingiliwa maji kutokana na mvua ya upepo. Hakuweza kuamka tena maji yakawa yanapita juu yake. Akabaki kukoroma.
Maskini Maureen bila kujitambua ni wapi hapo amelala aliendelea kulia lakini sauti yake haikusikiwa na yeyote yule hadi akanyamaza kimya. Alikuwa nusu amepoteza fahamu na nusu akiwa hai.
Hadi pale ulipofika wasaa wa kustaajabisha na kupigilia msumari katika kidonda kibichi.
Ni wakati Naomi na pombe zake kichwani akirejea nyumbani ndipo alimshuhudia Maureen lakini pombe ikamwongoza kuamini ni gunia, Naomi anashtuliwa na kunyanyuliwa ghafla kwa alichoamini kuwa ni gunia. Mwanga wa umeme uliokuwa umerejea dakika ile ndio ulimfungua akili Naomi, Maureen alikuwa amelala juu ya kifaa cha kusambaza umeme kutoka kwenye saketi ukutani, maji yalikuwa yamemuunganisha na umeme na sasa umeme ulikuwa ndani ya mwili wake ambapo ulimrusha ukutani. Kwa macho yake Naomi alimshuhudia Maureen akitulia tuli sakafuni, kwa ushahidi wa macho Naomi alitambua kuwa Maureen alikuwa kwenye tatizo kubwa sana na hiyo ilikuwa hatari kwa kibarua chake.
Hofu ikatanda. Hofu kuu.
* * * *
Hali ilikuwa tete sana asubuhi ile, hakuna aliyekuwa na jibu la tatizo hlo. Naomi alikuwa ameupanga uongo vizuri sana na kila mtu alikubaliana nae.
"Ni nini kimetokea" Walter akiwa na uoga waziwazi aliuliza swali hilo kwa kijana mmoja aliyekuwa anatokea kwenye eneo la tukio.
"Tanesco hao mh! Tanzania yetu hii dah!" alijibu huku akiendelea na safari yake.
"Samahan kaka Tanesco wamefanyaje kwani tafadhali" alihoji Walter. "Nenda kajionee kaka.." alijibu na kutoweka huku akitikisa kichwa kwa masikitiko makubwa. Aliutangaza uchungu waziwazi.
Walter na Mega walilazimika kuendelea kusogea mbele zaidi waweze kujua kuna nini, nguvu zilikuwa zinamwisha miguuni Walter, hakutaka kuruhuruhusu masikio yake kupokea taarifa mbaya itakayoharibu furaha aliyokuwa nayo kurudi Tanzania kusherekea sikukuu. Muga alikuwa katika sintofahamu, alishauzimisha muziki wake sasa alikuwa akivuta hatua moja baada ya nyingine ili wapate kujua ni kipi kimejiri katika nyumba ya nani.
"Dada samahani kuna nini?" Walter alimuuliza mwanadada mmoja aliyekuwa pekupeku. Huku usoni akiwa katika taharuki isiyofichika.
"Mh! sijui hata nielezeje lakini…ni Mungu tu…maskini dada wa watu." alianza kujibu kwa wasiwasi, akafumba macho kisha akatokwa na mguno mkubwa. Ni kama alikuwa haamini kilichotokea. Walter alikuwa katika kihoro cha kutambua kuna nini pale.
Hata kabla yule binti hajaanza kusimulia mkasa ule vizuri, macho ya Walter yalishuhudia mwili wa binadamu ukibebwa juu juu na wanaume watatu kuelekea kwenye gari ya wagonjwa iliyokuwa imefika pale, hakusubiri yule binti amalizie maelezo yake akaamua kutimua mbio kuelekea kwenye mwili ule aliamini kwa namna yoyote ile kuwa jibu la maswali yake anaenda kulipata pale, akiwa amebakiza takribani mita kumi kufika macho yake yanatua tena kwenye kundi la watu wakimgombeza mwanamke mmoja ambaye akili ya Walter ilimwambia kuwa anamfahamu, tatizo ni wapi amewahi kumuona?
"Ni nani yule nani kweli!" alianza kujiuliza akiwa amesahau kama alikuwa anawahi kutizama mwili uliobebwa ni wa nani na ni nini kimetokea. Watu waliokuwa wamemzunguka yule binti wengine walimuelewa na wengine hawakutaka kumwelewa kabisa,wengine walimsukuma wengne walimtetea. Hayo yote Walter hakutaka kuyajua alichotaka kufahamu ni wapi amemwona huyo binti, akiwa hajapata jibu alishtuliwa na ving’ora vya gari la wagonjwa barabarani tayari mwili ulishaingizwa na gari limeondoka.
Kama akili yake haikuathirika siku hiyo basi ni bahati, mbiombio akaanza kutimua mbio kuelekea nje tena akiachana na kundi lile alipokuwa yule dada aliyekuwa amemfananisha.
Walter alitaka kuliwahi lile gari la wagonjwa, hakuwa mtulivu kiakili na alitaka kuyajua mambo upesi upesi, kuna roho ilimsukuma waziwazi kuwa kuna jambo zito. Mbio za sakafuni huishia ukingoni, lakini mbio za utelezini huishia maangukoni.
Walter akiwa na moka yake ya bei ghali sana alikutana na utelezi mkali, akajaribu kuutafuta muhimili akaukosa, miguu ikatangulia kisha kisogo kikakutana na kitu kigumu sana.
Akili ikazimika palepale. Hakusema neno la ziada. Huu ukawa mwisho wa papara zake. Papara za kutaka kujua nini kimejiri.
Hii ikawa kesi nyingine watu wakahamia kwa Walter tena, Muga hadi dakika hiyo ni kama alikuwa amechanganyikiwa tayari kwa yote ambayo macho yake yalishuhudia ndani ya dakika chache. Akabaki kuhaha.
* * * *
NINI KINAENDELEA??
SEHEMU YA NNE
Maureen alikuwa amepigwa shoti kali ya umeme kutokana na kulala juu ya 'extension' bila kujua kisha maji ya kaingia na kumuunganisha na kile kifaa, ambapo umeme uliporejea yakamkumba maswahibu haya ya kusikitisha, shoti hiyo inazua walakini na utata kwa Naomi, msichana wa kazi ambaye anaujua ukweli lakini akaupindisha kujiweka salama.
Naomi hakuwa tayari kukiri kuwa alimuacha Naomi na kwenda zake katika viwanja vya starehe. Nafsini mwake alitambua wazi kuwa iwapo Maureen atakufa basi yeye ndiye muuaji kwa asilimia zote. Wazo hili lilimtesa sana na kujikuta akikosa amani.
Maswali anayoulizwa yanamchanganya na anajibu kwa kujichanganya, mwisho wa siku anaanza kuonekana muongo, wanaume wanamnasa makofi na wanawake wanamshikia bango. Hali tete.
Naomi anaiona hukumu mbele yake, hukumu ya kuuawa, anamkumbuka Mungu wake. Anamsihi aingilie kati ili apate nafasi nyingine ya kuishi kwa amani.
Ombi lake linakuja wakati muafaka. Ghafla mwanaume aliyekuwa anahaha huku na kule anateleza na kutulia tuli baada ya kuanguka. Waliokuwa wanamwandama wanakimbilia eneo la tukio.
Naomi anaupata upenyo wa kutoroka. Haipotezi baati hii.
Anatoweka.kimya kimya kuepusha tafrani mbele yake.
* * * * *
"Mbona niko hapa, gari la wagonjwa liko wapi? limembeba nani? da Maureen yuko wapi?" maswali mfululizo yalimtoka Walter baada ya kuzinduka na kujikuta kwenye kitanda hospitali. Nesi aliyekuwa pale hakuwa na jibu lolote lile.
"Naomi Naomi yule ni Naomi, Naomi wangu" Walter akaanzisha mkasa mwingine, nesi akadhani tayari mgonjwa ana matatizo ya akili. Mbiombio kaenda kumwita daktari, lakini kama vile alikuwa ameitwa Walter naye aliruka kutoka pale kitandani akatoka nje ya chumba cha hospitali huku akiwa na bandeji kichwani, kwa jinsi ambavyo hakuwa na hofu na wala hakutetemeka hata kidogo hakuna aliyeweza kumdhania kuwa alikuwa anatoroka hospitali. NESI alikuwa amefanya kosa kubwa sana kumwacha mgonjwa peke yake katika kile kitanda.
"Tabata shilingi ngapi?" Walter alikoroma mbele ya taksi.
"Buku saba mjomba"
"Nipeleke fasta!" alijibu Walter alipotajiwa bei na dereva taksi.
"Dah! nyie wagonjwa hamuaminiki nipe changu kwanza" akasema dereva yule wakati akianza kuiwasha gari yake.
Haraka haraka kwa kujiamini, Walter ambaye alionekana kuwa na haraka sana akazama mifukoni mwake, tofauti na matarajio yake hakukuta wallet yake mfukoni na aliambulia shiingi elfu mbili ya Uganda tu katika mfuko wake wa shati.
"Nilijua tu! yaani watu wengne bwana" alianza kuponda dereva alipogundua Walter hakuwa na kitu mfukoni. Walter hakuwa na hadhi tena mbele ya macho ya madereva wengine.
"Hapana nilikuwa na wallet kaka, sijui...."
"Huna lolote mzazi nenda ukapande daladala tena hizo zinapita!" alijibu dereva huku akimwonyesha Walter magari yanayotokea Muhimbili kwenda Buguruni. Walter kwa mfadhaiko mkubwa alisogea barabarani akapiga gari mkono akapanda japo lilikuwa limejaa.
"Yuko wapi mgonjwa!" daktari aliyefuatwa na nesi alihoji.
"Alikuwa hapa..." kwa uoga na kutetemeka alijibu nesi, kwani Walter hakuwepo tena pale.
"Maskini wa Mungu atakuwa ameenda wapi huyu kijana" alijiuliza daktari huku akijikuna kichwa chake.
****
Foleni ya siku hiyo ilikuwa ndefu sana tofauti na siku nyingine zote, kuanzia maeneo ya Magomeni gari alilopanda Walter lilikuwa halisogei mbele na tayari lilikuwa limezimishwa, abiria walikuwa wamekasirika mno na kila aina ya matusi kwa serikali yalisikika. Walter alikuwa mkimya sana, moyoni aliwaza mengi mazito, hakuwa hata na simu aweze kumpigia Muga wala Frank.
Akiwa ndani ya gari kuna mazungumzo yalimvutia kusikiliza.
"Jamani walikuwa wanamkimbiza hospitali na ajali imewazuia tena, mimi simlaumu dereva hata kidogo alikuwa anawahi" mama mmoja alikuwa akimwambia abiria mmoja katika gari alilokuwa amepanda Walter. Mama huyo aliyekuwa anatembea kwa miguu alionyesha huzuni yake dhahiri. Maneno hayo yalipokelewa kwa hofu na Walter, kwa wakati huo aliamini kila mgonjwa ni dada yake (Maureen) hivyo bila kujali jeraha lake kichwani alishuka na kuanza kujikongoja kuelekea kule alipotoka yule mama.
"Ni huyu ni huyu jamani" Walter alisikia maneno hayo nyuma yake lakini hakugeuka kwani macho yake yalikuwa yanatazama gari ya wagonjwa iliyogongwa vibaya ikiwa imeziba barabara. Huku akizidi kukaza mwendo alishtukia akikamatwa kwa nguvu na kufungwa kamba mikononi na miguuni.
Hakujua ni kwa nini kwani tayari alishasahau kuwa ametoroka hospitali
Ilimchukua dakika chache Walter kugundua tayari alikuwa mikononi mwa wauguzi na wahusika wa hospitali ambayo alikuwa ametoroka
"Jamani mimi ni mzima naenda kumwangalia dada yangu ni mgonjwa na alikuwa kwenye ile gari" aliongea Walter huku analia akiwaonyesha gari ya wagonjwa iliyokuwa imepata ajali mbaya sana. Wale watu hawakutaka kumwelewa waliamini amerukwa akili na hakujua anachokizungumza wakati ule. Kwa usalama wa maisha yake hawakumwachia.
"Jamani naomba mnielewe japo kidogo dada yangu anaitwa Maureen ndio namtafuta na mimi naitwa Walter hata nyie nafahamu ni wahusika wa hospitali sijachanganyikiwa mimi najitambua" alijaribu kwa kila hali Walter kuwashawishi watu hao kumwachia lakini badala yake walizidi kuimarisha ulinzi asiweze kupata nafasi ya kutoroka.
Walter hakuwa na njia mbadala hakuwa na nguvu za kuwazidi watu hawa hivyo alilazimika kwa shingo upande kukubali kupandishwa kwenye gari waliyokuja nayo watu hawa na kusubiri hadi foleni ilivyoanza kwenda akarudishwa hospitali alipochomwa sindano za usingizi na kufungwa mikono yake kikamilifu ili akizinduka asiweze kutoroka tena.
Fahamu zilipomrejea yalikuwa yamepita masaa kadhaa.
* * * * *
Ilikuwa taarifa ngumu sana kuingia na kukubalika katika kichwa cha Frank (baba mdogo wa Walter) pamoja na Anko Muga rafiki yake,taarifa ya gari aliyokuwa amepakizwa Maureen ili akimbizwe katika hospitali ya Muhimbili kutokana na hali yake kuzidi kuwa mbaya ilikuwa imepata ajali kwa kugongwa na gari kubwa upande wa ubavunh ambapo mwili wa mgonjwa ulirushwa nje ya gari "hali yake ni mbaya sana na foleni ni kubwa inashhndikana kuwahishwa hospitali,na hata madaktari waliopigiwa simu wafike haraka hawawezi kwa sababu ya foleni kubwa" ilimalizia kwa huzuni kubwa sauti ya mwanadada aliyekuwa anasoma habari ya ghafla ama mpasuko "BREAKING NEWS"katika kituo maarufu cha luninga hapa nchini.
"Walter atanielewaje mimi,huyo pekee ndiye ndugu yake aliyebaki hapa ulimwenguni!" Frank alijiuliza huku amejishika kichwa akitembea bila kujua anapoelekea hasa
"Frank nadhani si muda wa kujilaumu, tusubiri na Mungu atatuonyesha njia ya kweli labda atapona" Anko Muga alimpa matumaini Frank ambaye alionyesha kuchanganyikiwa kabisa kwa taarifa ile ya kushtusha. Nyumba yake ilikuwa shaghalabaghala aliamini umati uliofika pale siku ya tukio lazima walikuwepo vibaka hivyo alitegemea sana wizi pia umefanyika.
"Naomi yuko wapi?" ni swali la pekee aliloamini jibu lake lingemfungua akili yake, hakupata wa kumjibu Naomi hakuwa eneo lile tena,na hakuna aliyejua ameondoka sangapi pale, Frank alizidi kuchanganyikiwa.
Lakini hakuweza kuibadili siku hii. Hakuweza kuubadili ukweli uliopo.
Yaliyopangwa yakatimia.
* * * * *
"Ulale pema peponi Maureen, msalimie bibi mwambie mchumba wangu Naomi sijui alipo, wasalimie baba na mama waambie nawapenda sana, kwaheri dada Maureen"Aliongea hayo Walter wakati anauaga mwili wa Maureen uliokuwa umepondekapondeka vibaya kutokana na majanga aliyoyapata, kwanza umeme halafu ajali mbaya ya gari. Maneno na sauti yake vilimchoma kila mtu aliyeyasikia,Walter alikuwa na jeraha kisogoni, nguo zake zilikuwa chafu sana. Hakuhitaji kubadilisha na hakuwepo wa kuweza kumshawishi lolote.
"Nilitegemea kula nawe sikukuu za mwisho wa mwaka kwa nini hukusubiri lakini! Mbona hukutaka walau nipate dakika mbili za kukuona ukitabasamu. Ewe ardhi mwenye tamaa nimeze na mimi uridhike, hivi baba na mama hawakukutosha? Bibi naye je…haya na dadangu umemchukua….eeh Ardhi nimeze sasa hivi niondoke na Maureen" alishindwa kujizuia Walter akaangua kilio kikali, wakati huo Frank alikuwa hajiwezi ameishiwa nguvu akiwa amekaa chini, ulikuwa msiba ulioteka hisia za wengi sana katika mitaa mbalimbali jijini Dar-es salaam.
Kilio cha mtu mzima kikachukua nafasi.
ITAENDELEA.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Urusi: Vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini havitafua dafu

MTEULE THE BEST Image caption Waziri wa maswala ya kigeni nchini Urusi Sergei Lavrov na mwenzeka wa Marekani Rex Tillerson Waziri wa maswala ya kigeni nchini Urusi Segei Lavrov amemwambia waziri wa ulinzi nchini Marekani Rex Tillerson kwamba kuiwekea vikwazo zaidi Korea Kaskazini hakutafua dafu. Taarifa iliochapishwa na wizara ya kigeni nchini Urusi inasema kuwa wawili hao walizungumza kwa njia ya simu na kushutumu majaribio ya makombora ya hivi karibuni yaliotekelezwa na Pyongyang . Lakini inasema kuwa bwana Lavrov alisisitiza kwamba diplomasia ndio njia ya pekee ya kumaliza wasiwasi katika rasi ya Korea, na kutaka hatua zozote dhidi ya taifa hilo kusitishwa akionya huenda zikasababisha madhara yasiojulikana. Waziri wa ulinzi nchini Marekani amesisitiza kuwa bado kuna fursa ya kidiplomasia katika kukabiliana na Korea Kaskazini. Mapema rais Trump alichapisha ujumbe katika akaunti yake ya Twitter akisema mazungumzo sio suluhisho.

*DKT. MAGUFULI, MNANGAGWA WAWEKA HISTORIA MPYA*

Rais wa Zimbabwe, Emerson Mnangagwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Zimbabwe, Emerson Mnangagwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli wameweka historia mpya kwa kukubaliana kushirikiana kwenye maeneo makuu matatu yenye tija pande zote. *Kwanza*, *Kuimarisha uchumi* wa nchi hizi mbili kwa kukuza uwekezaji na biashara ambao umeanza kuonesha matunda makubwa. Mathalani, katika eneo la biashara kumeonyesha mafanikio makubwa kila mwaka. Mfano mwaka 2016 biashara kati ya Tanzania na Zimbabwe ilikuwa ni Tsh. Bilioni 18.3. Mwaka 2017 biashara ilikuwa Tsh. Bilioni 21.1. *Pili*; *kushirikiana* vyema kwenye masuala ya *utalii* kwa kutumia wingi wa vivutio vya utalii kama vile mbuga za wanyama, fukwe, maeneo ya kihistoria pamoja na Mlima Kilimanjaro. *Tatu*; Kushirikiana na kuimarisha eneo la *huduma za kijamii* zikiwemo afya, utamaduni, elimu na kukuza lugha ya kiswahili ambapo Tanzania ina Waalimu wa kutosha na hivyo...

MAPENZI: Kuna faida na ni muhimu Mpenzi wako kuwa rafiki yako pia

Kuna faida kubwa kwa wapenzi kuwa marafiki KUTOKANA na mila mbalimbali, baadhi ya watu wamekuwa wakiamini kwamba mwanamke ni daraja la pili. Daraja la kwanza na lenye kuthaminiwa ni mwanaume. Yaani mwanamke hana kauli kwa mwanaume. Anakuwa kama mtumwa fulani hivi.  Mwanaume akiongea, basi ni maelekezo kama vile rais wa nchi anavyotoa maelekezo kwa watu walio chini yake. Hakuna wa kupinga. Akisema sitaki kitu fulani kifanyike, basi ni mpaka atakapotoa maelekezo mengine. Vinginevyo, maelekezo ya awali yatabaki kusimama kama sheria.  Wapo baadhi ya wanawake wanaofurahia aina hii ya uhusiano kwa sababu ya mazoea. Kwamba wamekuzwa hivyo, mwanaume ni mwanaume. Huu ni mfumo ambao watu wengi wamekuwa wakiuishi. Kuna ambao wanakubaliana nao, wengine hawakubaliani nao.  Watu wengi sana wamekuwa wakiishi katika malumbano katika mahusiano yao kutokana na mfumo huu wa maisha. Mwanamke hataki kuishi kama mtumwa, mume anakomaa kuonesha uanaume wake. Hakuna anayekubali kushuka,...