MTEULE THE BEST
Wabunge wa Ujerumani wataka wahamiaji waliokataliwa wafukuzwe haraka
Wabunge wa Ujerumani wametoa mwito wa kuharakishwa kwa mchakato wa kuwafukuza wahamiaji wanaokataliwa hifadhi nchini
Mji wa Ansbach baada ya mashambulio ya Jumapili
Mbunge wa chama kinachoongoza serikali ya mseto CDU, Armin Schuster amesema Ujerumani inapasa pia kuwa na tabia ya kusema kwaheri, na sio ya kukaribisha tu.
Bwana Schuster ameeleza katika mahojiano na magazeti muhimu ya nchini Ujerumani kwamba Ujerumani imeshindwa kuitekeleza kanuni ya kuwafukuza haraka wahamiaji, baada ya maombi yao ya kuishi nchini kukataliwa.
Bwana Schuster ambae pia ni mtaalamu wa masuala ya ndani ya nchi bungeni, amefahamisha kwamba bado wapo wahamiaji zaidi ya laki nchini Ujerumani, ingawa maombi yao ya kuishi nchini yamekataliwa.
Naye Mbunge wa chama cha mrengo wa kushoto Sarah Wagenknecht ameikosoa sera ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel juu ya wakimbizi.
Amesema matukio ya siku za hivi karibuni yamethibitisha kwamba kupokea idadi kubwa ya wakimbizi wanaohitaji kushughulikiwa ni changamoto kubwa na kazi ngumu kuliko Kansela Merkel anavyojaribu kusema kwamba atafanikiwa.
Mkimbizi kutoka Syria ajilipua
Wabunge wa Ujerumani wameutoa mwito huo wa kuwafukuza haraka wakimbizi wanaonyimwa ruhusa ya kuishi nchini baada ya kutokea mashambulio mengine katika mji wa Ansbach katika jimbo la Bavaria, la kusini mwa Ujerumani Jumapili iliyopita.
Mkimbizi mmoja kutoka Syria alijilipua baada ya maombi yake ya kupatiwa hifadhi nchini kukataliwa. Mtu huyo alijilipua na kujiua karibu na klabu ya burudani na kuwajeruhi watu wengine 15. Kabla ya kulifanya shambulio hilo mtu huyo aliekuwa na umri wa miaka 27,aliapa utiifu kwa kiongozi wa kundi la magaidi wanaojiita Dola la Kiislamu.Alifyatua bomu lililokuwamo ndani ya shanta- kifuko cha mgongoni.
Kwa mujibu wa maafisa,ukanda wa video wa mtu huyo uliopatikana baadae ulibainisha azma yake ya kuishambulia Ujerumani,ili kulipiza kisasi kwa sababu ya nchi hiyo kuupinga Uislamu.
Maafisa wa idara husika wamefahamisha kwamba mshambuliaji huyo aliwasili nchini Ujerumani miaka miwili iliyopita lakini maombi yake ya kupatiwa hifadhi ya ukimbizi nchini yalikataliwa na alipangiwa kuondolewa na kurudishwa Bulgaria ambako aliingia kwanza na kusajiliwa.
Hata hivyo waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere amesema mpango wa kumfukuza mtu huyo ulisimamishwa kwa muda kutokana na matatizo ya kiakili aliyokuwanayo. Lakini idara za jimbo la Bavaria zimearifu kwamba mshambuliaji huyo alikuwa tayari ameshapokea amri ya kuondoka nchini wiki mbili kabla ya kadhia ya Jumapili iliyopita.Ilikuwa afukuzwe nchini mnamo muda wa siku 30.
Mwandishi:Mtullya abdu/ZA,DW
Maoni