YAH: KURUDISHA FEDHA (TZS MILIONI 40.4) NILIZOPEWA NA NDUGU JAMES RUGEMALIRA WA KAMPUNI YA VIP ENGINEERING AND MARKETING LTD.
1. Kama inavyokumbukwa, kutokana na ukweli kwamba ilisharipotiwa sana kwenye vyombo vya habari, kwamba tarehe 12/02/2014 nilipokea fedha kiasi cha shilingi milioni 40.4 za kitanzania kutoka kwa Ndugu James Rugemalira, mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd. Fedha hizo nilizipokea kupitia akaunti yangu namba 00110102352601 ya Benki ya Mkombozi.
2. Fedha hizo nilizipokea, kwa nia njema, kama msaada/mchango kutoka kwa ndugu Rugemalira ili zinisaidie katika kutimiza majukumu yangu ya kibunge, hususan,kusaidiana na wananchi wa jimbo langu la Sengerema na Taifa kwa ujumla, kutekeleza shughuli za kijamii (mfano ujenzi wa makanisa, misikiti, kusaidia kulipia karo za wanafunzi wasiojiweza, n.k) na shughuli za miradi ya maendeleo ambayo haipo kwenye bajeti ya serikali.
3. Nilipokea Fedha hizo kutoka kwa ndugu Rugemalira bila kujua kwamba fedha hizo zilikuwa zinahusishwa na kashfa ya akaunti ya fedha za Escrow kama ilivyo sasa.
4. Fomu ya Tamko langu kama kiongozi wa umma kuhusu rasilimali na madeni kwa mujibu wa sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995 kwa kipindi kilichoishia 31 Desemba, 2014, niliyoiwasilisha ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma tarehe 24/12/2014 ilijumuisha msaada huu wa shilingi milioni 40.4 kutoka kwa ndugu James Rugemalira.
5. Tarehe 15/01/2015 nililipa kodi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kiasi cha Shilingi 13,138,125/= ikiwa ni sawa na asilimia 30 (30%) ya msaada huo niliopewa, kama ilivyoelekezwa na TRA.
SABABU ZA KURUDISHA FEDHA HIZI.
i) Nilipokea msaada huu kama wapokeavyo wabunge wengine, kwa nia njema, bila kujua kwamba James Rugemalira baadaye angekuja kuhusishwa na kashfa ya fedha za akaunti ya ESCROW kama ilivyo sasa.
ii) Kwa vile sasa imedhihirika kwamba aliyenipa msaada huu anatuhumiwa kwenye kashfa ya akaunti ya ESCROW, nimepima na kutafakari, na hatimaye nimeamua, kwa hiari yangu mwenyewe, kurejesha serikalini (TRA) fedha zote nilizopewa kama msaada (TZS milioni 40.4) bila kujali kwamba nilishazilipia kodi ya mapato kama nilivyoeleza hapo awali. Risiti ya ushahidi wa kurejesha fedha hizi serikalini hii hapa.
iii) Nimeamua kurejesha fedha hizi hata kama aliyenipa msaada bado ni mtuhumiwa tu, kwa vile hajathibitika kupatikana na hatia, kwa sababu sitaki kuwa sehemu ya kashfa/tuhuma hizo.
iiii) Leo nina zaidi ya miaka 12 nikiwa kiongozi wa Umma, na pia niliwahi kuitumikia wizara ya Nishati na Madini kwa takribani miaka mitano na nusu ( Naibu Waziri/Waziri), lakini sijawahi kukumbwa na kashfa ya rushwa au ufisadi. Kwa hiyo nimesononeka na kufadhaika sana kuona kuwa msaada niliopewa sasa unahusishwa na tuhuma.
v) Ninarudisha fedha hizi ili kulinda heshima na maslahi mapana ya nchi yangu, chama changu (CCM), Serikali yangu, Jimbo langu la Sengerema, familia yangu na heshima yangu mwenyewe.
HITIMISHO
• Kupokea msaada ni jambo la kawaida, ila ikibainika kuwa msaada unaopewa una harufu ya uchafu hata kama haujathibitishwa na vyombo husika ni vyema kujiepusha nao.
• Ninampongeza, kwa dhati kabisa, Rais wetu mpendwa Dr John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya kwa maslahi ya Taifa letu. Nami naungana na watanzania wenzangu wazalendo kumuombea kwa Mungu na namhakikishia nitaendelea kumuunga mkono kwa kupigania maendeleo ya nchi yetu.
Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania
William Mganga Ngeleja (Mb)
Jimbo la Sengerema
10/07/2017
Maoni