Ruka hadi kwenye maudhui makuu

Generali azungumzia kamatakamata ya viongozi wa upinzani

MTEULE THE BEST

Tansania Jenerali Ulimwengu Journalist (privat)

Sasa limekuwa ni jambo la kawaida la kila siku watu kushuhudia kiongozi wa upinzani akikamatwa na polisi kwa tuhuma za makosa yasiyokuwemo katika vitabu vya sheria nchini Tanzania. Ni jambo ambalo limeanza kuzoeleka kwamba wawakilishi wa wananchi ā€“ wabunge au madiwani ā€“wanaweza kushikiliwa na vyombo vya usalama bila kujali kabisa wadhifa wao ndani ya jamii wala usahihi wa tuhuma zinazoelekezwa kwao, anasema Jenerali Ulimwengu.
Katika shauri mojawapo, mbunge wa Arusha, Godbless Lema, aliwekwa mahabusu na kushikiliwa kwa muda wa miezi minne bila maelezo yo yote. Hatimaye alipewa dhamana na mahakama ya rufani ambayo iliwakaripia mahakimu wa mahakama za chini pamoja na mawakili wa upande wa mashitaka kwa kile ilichokiita ā€˜kunajisi sheriaā€™ kwa kuwanyima watuhumiwa dhamana, ambayo ni haki yao ya msingi kabisa.
Ingawaje Lema aliruhusiwa dhamana, amekuwa akilazimika kuhudhuria mahakama mara kwa mara kwa ajili ya kesi zinazomkabili ambazo zinahusu madai ya uchochezi.
Mbunge mmoja wa kike jimboni Bunda, mkoani Mara, Esther Bulaya, ameshikiliwa na polisi kwa kushukiwa kutaka kuandaa mkutano wa hadhara nje ya jimbo lake. ā€˜Kosaā€™ hili la kushangaza linatokana na amri ya mwaka jana iliyotolewa na Rais John Magufuli kuwazuia wanasiasa kufanya mikutano ya hadhara nje ya majimbo yao ya uchaguzi. Kwamba hakuna sheria inayosema hivyo haionekani  kuwasumbua  askari-polisi, ambao wanayachukulia matamko ya rais kama sheria ya Bunge.
Tundu Lissu ni mbunge na mwanasheria wa Chadema, chama cha upinzani, na pia ni rais wa Chama Cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS). Hivi sasa amegeuka kuwa mtuhumiwa anayeshikwa mara nyingi zaidi kuliko wengine akituhumiwa kwa mlolongo wa tuhuma, kutoka ā€˜kumtusi raisā€™ hadi ā€˜kutoa matamko ya uchocheziā€™. Lissu amekuwa akimwita Rais Magufuli ā€˜dikteta uchwara,ā€™ na hivi karibuni aliingia matatani tena baada ya kujaribu kudhihirisha kwamba Magufuli, alipokuwa waziri wa ujenzi, alichukua maamuzi yaliyosababisha hasara kubwa kwa serikali.
Tansania - Tundu Lissu (DW)
Tundu Lissu akiwasili mahakamani kusikilia kesi yake
Lissu alichaguliwa kuwa rais wa TLS baada ya Magufuli kueleza kutokupendezwa kwake na chama hicho cha mawakili kuendeshwa na wanasiasa. Tamko la Magufuli lilichochea hamasa kubwa za wanasheria kutoka kila upande wa nchi waliojazana mjini Arusha kumpa Lissu ushindi. Baada ya Lissu kuchaguliwa kwa kishindo, waziri wa serikali alitishia kuifuta TLS, ambacho ni chama cha kitaaluma kilichoanzishwa chini ya sheria za Bunge na chenye uhusiano rasmi wa kikazi na serikali.  
Karibu kila siku kuna mwanasiasa wa upinzani anayeamuriwa kupiga ripoti polisi au kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma mbali mbali. Chadema kimedai kwamba tangu Magufuli aingie madarakani zaidi ya viongozi 400 wa Chadema wameshitakiwa kwa tuhuma za kubuni, na mara nyingi wamenyimwa dhamana.
Kwa jinsi ambavyo wanasiasa wa upinzani wanavyobughudhiwa na polisi, na kuitwa mara kwa mara vituoni kutoa maelezo, mtu mmoja ameshauri wapinzani wafungue tawi dogo katika vituo vya polisi ili waweze kuendesha shughuli zao kwa urahisi zaidi. 
Chama kingine cha upinzani, Civic United Front (CUF), kimeingia katika mgogoro wa kiuongozi ambao wengi wanaamini unachochewa na serikali. Mgogoro mkubwa ni kati ya Profesa Ibrahim Lipumba, (mwenyekiti aliyejiuzulu kisha akabadili uamuzi wake na kudai kurejea katika nafasi hiyo), na Seif Sharif Hamad, ambaye ni katibu mkuu wa CUF na mpinzani wa siku nyingi mwenye ushawishi mkubwa za kisiasa visiwani Zanzibar 
Katika mvutano huo, asasi za kiserikali zinaonekana kumuunga mkono Profesa. Msajili wa vyama vya siasa ameonyesha kubariki kufukuzwa kwa wabunge waliomuunga mkono Hamad na pia ameidhinisha Lipumba apewe fedha za ruzuku ambazo ni halali ya CUF.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MAPENZI: Kuna faida na ni muhimu Mpenzi wako kuwa rafiki yako pia

Kuna faida kubwa kwa wapenzi kuwa marafiki KUTOKANA na mila mbalimbali, baadhi ya watu wamekuwa wakiamini kwamba mwanamke ni daraja la pili. Daraja la kwanza na lenye kuthaminiwa ni mwanaume. Yaani mwanamke hana kauli kwa mwanaume. Anakuwa kama mtumwa fulani hivi.  Mwanaume akiongea, basi ni maelekezo kama vile rais wa nchi anavyotoa maelekezo kwa watu walio chini yake. Hakuna wa kupinga. Akisema sitaki kitu fulani kifanyike, basi ni mpaka atakapotoa maelekezo mengine. Vinginevyo, maelekezo ya awali yatabaki kusimama kama sheria.  Wapo baadhi ya wanawake wanaofurahia aina hii ya uhusiano kwa sababu ya mazoea. Kwamba wamekuzwa hivyo, mwanaume ni mwanaume. Huu ni mfumo ambao watu wengi wamekuwa wakiuishi. Kuna ambao wanakubaliana nao, wengine hawakubaliani nao.  Watu wengi sana wamekuwa wakiishi katika malumbano katika mahusiano yao kutokana na mfumo huu wa maisha. Mwanamke hataki kuishi kama mtumwa, mume anakomaa kuonesha uanaume wake. Hakuna anayekubali kushuka,...

Urusi: Vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini havitafua dafu

MTEULE THE BEST Image caption Waziri wa maswala ya kigeni nchini Urusi Sergei Lavrov na mwenzeka wa Marekani Rex Tillerson Waziri wa maswala ya kigeni nchini Urusi Segei Lavrov amemwambia waziri wa ulinzi nchini Marekani Rex Tillerson kwamba kuiwekea vikwazo zaidi Korea Kaskazini hakutafua dafu. Taarifa iliochapishwa na wizara ya kigeni nchini Urusi inasema kuwa wawili hao walizungumza kwa njia ya simu na kushutumu majaribio ya makombora ya hivi karibuni yaliotekelezwa na Pyongyang . Lakini inasema kuwa bwana Lavrov alisisitiza kwamba diplomasia ndio njia ya pekee ya kumaliza wasiwasi katika rasi ya Korea, na kutaka hatua zozote dhidi ya taifa hilo kusitishwa akionya huenda zikasababisha madhara yasiojulikana. Waziri wa ulinzi nchini Marekani amesisitiza kuwa bado kuna fursa ya kidiplomasia katika kukabiliana na Korea Kaskazini. Mapema rais Trump alichapisha ujumbe katika akaunti yake ya Twitter akisema mazungumzo sio suluhisho.

Fuvu la binadamu wa kale liligunduliwa miaka 60 iliyopita nchini Tanzania

Fuvu la binadamu wa kale liligunduliwa miaka 60 iliyopita nchini Tanzania Miaka 60 siku kama ya leo ugunduzi mkubwa ulifanyika katika eneo la Olduvai Gorge, kwenye kreta ya Ngorongoro. Wanaakiolojia Louis na Mary Leakey waligundua fuvu la mtu anayeaminika kuwa ni wa kale zaidi waliyompa jina la Zinjanthropus. Ugunduzi huo uliofanyika saa nne asubuhi Julai 22, 1959 kipindi hicho kwenye eneo la Tanganyika ulikuwa wa vipande zaidi ya 100 ukasaidia katika kutambua asili ya watu wa awali duniani. Kabla ya ugunduzi huo, wanasayansi na wanahistoria walikuwa wakiamini kuwa binadamu wa kale walitokea Uchina baada ya ugunduzi wa mafuvu ya kale baina ya 1923 na 1927 nchini humo ya Homo eractus, ama maarufu kama Peking Man. Mafuvu hayo ya Uchina yalikuwa na umri wa takribani miaka 750,000. Mafuvu ya Olduvai eneo ambalo kwa sasa lipo Tanzania wakati wa ugunduzi wake lilikuwa na umri wa takribani miaka milioni 1.75, na hakuna mabaki ya mtu wa kale zaidi ambayo mpaka sasa yamegundul...