MTEULE THE BEST
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametoa wito wa kutafakari upya mtazamo wa serikali ya Ujerumani kuelekea Uturuki baada ya nchi hiyo kuwakamata raia wawili zaidi wa Ujerumani.
Uhusiano kati ya nchi hizo mbili umeporomoka tangu jaribio lililoshindwa la mapinduzi mwaka 2016.
Hakuna "msingi wa kisheria" wa kukamatwa katika matukio mengi, Merkel amesema , akielezea kuhusu Wajerumani wawili waliokamatwa siku ya Alhamis nchini Uturuki, na kufikisha jumla ya idadi ya raia wa Ujerumani waliokamatwa nchini humo kwa sababu za kisiasa kuwa 12.
"Hii ndio sababu tunahitaji kuchukua hatua muhimu hapa," amesema , na kuongeza kwamba serikali "huenda inapaswa kutafakari upya" uhusiano wake na Uturuki.
Deniz Yucel (kushoto) mwandishi habari raia wa Ujerumani mwenye asili ya Uturuki
Merkel amesema Ujerumani tayari, "imeendeleza kwa kiasi kikubwa " uhusiano wake na Uturuki, lakini hatua hii mpya ina maana "huenda ni muhimu kutafakari upya zaidi," na kuongeza kwamba kunaweza kuwa na mazungumzo zaidi juu ya ushiriki wa Ankara katika Umoja wa forodha wa Umoja wa Ulaya hadi pale hali ya hivi sasa itakapotatuliwa.
"Madai yetu kwa Uturuki yako wazi kabisa," msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Seibert amesema. "Tunatarajia Uturuki itawaachia huru raia wa Ujerumani ambao wamekamatwa kwa misingi isiyokuwa ya kisheria."
Mahusiano baina ya washirika hao wa NATO yamevurugika tangu pale serikali ya Ujerumani ilipoikosoa Uturuki kuhusiana na ukandamizaji uliofuatia jaribio la mwaka jana lililoshindwa la mapinduzi.
Kukamatwa Wajerumani
Kukamatwa kwa Wajerumani wawili siku ya Alhamis kunafikisha idadi ya watu 55, Wajerumani waliokamatwa nchini Uturuki, 12 kati yao wanashikiliwa kwa sababu za kisiasa na wengine wanne wana uraia pacha wa Ujerumani na Uturuki , ikiwa ni pamoja na mwandishi habari mwenye uraia wa Uturuki na Ujerumani Deniz Yucel, ambaye yuko kizuwizini sasa kwa siku 200, imesema wizara ya mambo ya kigeni ya Ujerumani.
Shirika la habari la Uturuki linaloendeshwa na serikali Anadolu limeripoti kwamba raia wawili wa Ujerumani wenye asili ya Uturuki wamekamatwa katika uwanja wa ndege wa Antalia kwa madai ya kuwa na uhusiano na mtandao wa imamu anayeishi uhamishoni nchini Marekani Fethullah Gulen , ambaye Ankara inamshutumu kwa kutayarisha jaribio la mapinduzi lililoshindwa mwaka jana.
Kiongozi wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan
Ujerumani haijafahamishwa rasmi kuhusiana na kukamatwa kwa watu hao wawili, ambako kulitokea katika uwanja wa ndege wa Antalia siku ya Alhamis.
Ubalozi mdogo wa Ujerumani katika mji wa pwani wa Izmir ulifahamishwa kuhusu kukamatwa huko "na vyanzo ambavyo si vya serikali," msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Maria Adebahr aliwaambia waandishi habari.
"Tunajaribu kujua wanashitakiwa kwa madai gani," amesema Adebahr. "Tunapaswa kufikiria kwamba ni madai ya kisiasa, shaka ya ugaidi, kama ilivyo kwa wengine."
Wanadiplomasia hawajaweza kuwa na mawasiliano nao , ameongeza, sikukuu ya Ijumaa ya Kiislamu ya Eid al-Adha ikiwa ni sababu mojawapo ya uchelewesho wa mawasiliano na maafisa.
- Pata kiungo
- X
- Barua pepe
- Programu Nyingine
Maoni