MTEULE THE BEST
Mapema asubuhi, mnamo 30 Oktoba 1961, ndege ya kuangusha mabomu ya Muungano wa Usovieti aina ya Tu-95 ilipaa kutoka uwanja wa kambi ya ndege za kivita ya Olenya katika rasi ya Kola kaskazini mwa Urusi.
Tu-95 ilikuwa ndege kubwa sana yenye injini nne ambayo iliundwa mahsusi kubeba mabomu.
Katika mwongo mmoja uliotangulia, Muungano wa Usovieti ulikuwa umepiga hatua sana katika utafiti kuhusu nyuklia.
Marekani na USSR zilikuwa zimejipata upande mmoja wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia lakini baada ya vita, kukatokea Vita Baridi.
Wasovieti baada ya kujipata wanakabiliwa na taifa pekee lililokuwa na silaha za nyuklia, iliona njia pekee ya kushindana vyema na Marekani ilikuwa ni kuwa na silaha zake za aina hiyo.
Tarehe 29 Agosti 1949, Wasovieti walikuwa wamefanyia majaribio silaha yake ya kwanza ya nyuklia kwa jina 'Joe-1' katika eneo ambalo sasa linapatikana Kazakhstan.
Walitumia ujuzi uliopatikana kwa kuingia kisiri na kupata taarifa kuhusu mpango wa atomiki wa Marekani.
Katika miaka iliyofuata walikuwa wamepiga hatia sana. Walikuwa wamelipua silaha zaidi ya 80 za atomiki kipindi hicho. Mwaka 1958 pekee, Wasovieti walikuwa wamefanyia majaribio mabomu 36 ya nyuklia.
Lakini hakuna bomu hata moja walilokuwa wamefanyia majaribio awali ambalo lilikaribia bomu lililokuwa limebebewa na ndege hiyo aina ya Tu-95.
Lilikuwa bomu kubwa sana, bomu ambalo halingetoshea sehemu ya kubebea mabomu ya ndege.
Bomu hilo lilikuwa na urefu wa 8m (26ft), kipenyo cha karibu 2.6m (7ft) na lilikuwa na uzali wa tani 27.
Muonekano wake ulikuwa sawa na mabomu yaliyopewa majina 'Little Boy' na 'Fat Man' ambayo yalikuwa yameangushwa na Marekani katika miji ya Hiroshima na Nagasaki miaka kumi na mitano awali.
Bomu hilo lilifahamika kwa majina mengi sana kiufundi - kuna walioliita Project 27000, Product Code 202, RDS-220, na Kuzinka Mat (Mamake Kuzka).
Lakini sasa hufahamika zaidi kama Tsar Bomba - 'Bomu la Tsar'.
Tsar Bomba halikuwa bomu la kawaida la nyuklia.
Lilikuwa matunda ya jaribio la wanasayansi wa USSR la kuunda silaha ya nyuklia yenye nguvu zaidi duniani wakati huo.
Aidha, walitiwa hamasa na hamu ya waziri Mkuu Nikita Khruschchev ya kutaka kuwa na silaha ambayo ingeufanya ulimwengu kutikiswa na 'kunyenyekea' kutokana na teknolojia ya silaya ya Muungano wa Usovieti.
Ilikuwa zaidi ya kifaa cha chuma ambacho hakingetoshea ndani ya sehemu ya kubebea mabomu ya ndege kubwa zaidi ya kivita - ilikuwa ni silaha ya maangamizi makubwa, silaha ya kutumiwa wakati wa mwisho kabisa.
Ndege hiyo ya Tupolev (Tu) ilikuwa imepangwa rangi nyeupe kupunguza madhara ya mwanga ambao ungezalishwa na mlipuko wa bomu hilo.
Ndege hiyo ilifika eneo la kuangushwa bomu Novya Zemlya, eneo ambalo halikuwa na watu katika visiwa vya Bahari ya Barents juu katika kaskazini maeneo yenye barafu ya USSR.
Rubani wa ndege hiyo ya Tupolev Meja, alifikisha ndege hiyo Ghuba ya Mityushikha Bay, eneo la kufanyia majaribio silaha la muungano wa Usovieti na kufika karibu 34,000ft (10km) juu angani. Ndege nyingine ya kuangusha mabomu aina ya Tu-16 ilipaa karibu na ndege yake, lengo lake likiwa kupiga video mlipuko wa bomu hiyo na kuchunguzaathari za mlipuko huo hewani ikipitia eneo la mlipuko.
Ili kuhakikisha ndege hizo mbili haziharibiwi - na uwezekano wa kutodhurika ulikuwa asilimia 50 - ilipangwa kwamba Tsar Bomba iangushwe kwa parachute ya uzani wa karibu tani moja.
Bomu hiyo lingeshuka hadi kiwango kilichotakikana- 13,000ft (3,940m) - na kisha kulipuka.
Wakati wa mlipuko, ndege hizo za kuangusha mabomu zingekuwa karibu 50km (30 miles) mbali na eneo hilo. Umbali huo ungetosha kuzuia ndege hizo kuathirika.
Tsar Bomba ililipuliwa saa 11:32, saa za Moscow. Ghafla, bomu hilo lililipuka na kusababisha moto mkubwa wa upana wa karibu maili tano. Moto huo ulipaa angani kutoka eneo la mlipuko kutokana na nguvu za mlipuko wenyewe. Mwanga wa mlipuko huo ungeonekana na watu waliokuwa umbali wa 1,000km (maili 630).
Wingu la mlipuko lililofanana na uyoga lilipaa juu hadi 64km (40 miles), sehemu ya juu ikiwa imepanuka kwa karibu 100km (maili 63) kuanzia sehemu moja hadi nyingine. Kilikuwa kitu cha kushangaza sana bila shaka.
Katika eneo la Novaya Zemlya, madhara ya bomu hilo yalikuwa ya kuogofya.
Katika kijiji cha Severny, 55km (maili 34) kutoka eneo la mlipuko, nyumba zote ziliharibiwa kabisa.
Hii ni sawa na nyumba zote zilizo katika uwanja wa ndege wa Gatwick nchini Uingereza zikiharibiwa na mlipuko uliotokea katikati mwa London.
Katika wilaya za Muungano wa Usovieti zilizokuwa mamia ya maili mbali na eneo la mlipuko, uharibifu wa kila aina ulitokea. Nyumba ziliporomoka, mapaa ya nyumba yakaanguka, vioo kwenye madirisha vikavunjika na milango ikaharibika pia.
Mawasiliano ya redio yalitatizika kwa zaidi ya saa moja.
Durovtsev na ndege yake ya Tupolev walikuwa na bahati kunusurika - mlipuko wa bomu hilo ulisababisha ndege hiyo kushuka ghafla zaidi ya 1,000m (3,300ft) kabla ya rubani huyo kuweza kuidhibiti tena.
Mpiga picha wa Usovieti aliyeshuhudia mlipuko huo alisema baadaye:
"Mawingu chini ya ndege na maeneo ya mbali yalitiwa mwanga na nuru ya ghafla yenye nguvu. Mwanga huo ulienea na kuwaka hivi kwamba ungeweza kuona ndani ya mawingu. Wakati huo, ndege yetu ilitokea kutoka katikati ya mawingu mawili na chini kitu kilichofanana na mpira cha rangi iliyokolea ya machungwa kilikuwa kinajitokeza. Kilikuwa cha kuogofya na kilifanana na sayari ya Jupiter. Aste aste, kilianza kupaa juu. Kilionekana kana kwamba kilikuwa kinaimeza Dunia. Lilikuwa tukio la kushangaza sana, sijawahi kuliona.
Tsar Bomba ilizalisha nishati ambayo nguvu zake zilikuwa haziwezi kufikirika.
Kwa sasa, inasadikiwa kwamba bomu hilo lilizalisha nishati ya megatani 57 au sawa na tani milioni 57 za TNT. Hiyo ni mara 1,500 zaidi ya mlipuko wa mabomu ya Hiroshima na Nagasaki kwa pamoja.
Aidha, ni mara kumi zaidi ya nguvu za mabomu yote ambayo yalilipuliwa wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Mlipuko kama huo haungewekwa siri.
Ndege ya kijasusi ya Marekani iliyokuwa kilomita elfu kadha kutoka eneo hilo, ilikuwa na kifaa cha kupima milipuko ya nyuklia kwa mbali.
Takwimu kutoka kwa ndege hiyo zilitumiwa na wataalamu wa jopo la kufuatilia silaha za nchi za nje la Marekani kukadiria uwezo wa bomu hilo.
Muda si muda, mataifa yalianza kushutumu kitendo hicho cha USSR.
Marekani na Uingereza, na hata nchi za Ulaya majirani wa muungano huo mfano Sweden.
Bahati pekee ni kwamba wingu la mlipuko huo halikuwa limefika ardhini, jambo lililosababisha kiwango cha miali nururishi iliyotokana na bomu hilo kuwa chini sana.
Hali ingekuwa tofauti sana kama hilo lingetokea.
Ni bahati kwani bomu hilo lilikuwa limefanyiwa mabadiliko kidogo kupunguza uwezo wake. Tsar Bomba ilikuwa imeundwa kuwa na uwezo mara mbili ya uliokuwa kwenye bomu hilo lilipolipuliwa.
Mmoja wa waliohusika zaidi kuunda bomu hilo alikuwa mwanafizikia Andrei Sakharov ambaye baadaye alipata umaarufu sana kwa kuongoza juhudi za kumaliza silaha za nyuklia - ambazo alikuwa mwenyewe amechangia kuziunda na kuzistawisha.
Maoni