Iran inataka mataifa ya Ulaya kuwafidia ifikapo mwisho wa mezi Mei baada ya Marekani kujiondoa kwenye mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015, kwa mujibu wa afisa mwandamizi. Iran itaamua iwapo itasalia kwenye mpango huo.
Makubaliano ya mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa yenye nguvu ulimwenguni yaliondoa vikwazo dhidi ya Iran huku taifa hilo likitakiwa kusitisha mpango wake wa nyuklia.
Tangu Rais Donald Trump aiondoe Marekeni kwenye makubaliano hayo mwezi uliopita, mataifa ya Ulaya yamekuwa yakijaribu kuhakikisha kuwa Iran inafaidika kiuchumi ili kuishawishi kuendelea kusalia kwenye mwafaka huo. Lakini jambo hilo linasalia kuwa changamoto baada ya kampuni za Ulaya kutishwa na vikwazo vya Marekani.
Mataifa yaliyosalia kwenye mwafaka huo yanakutana Ijumaa (25.05.2018) kwa mara ya kwanza tangu Trump kujindoa kwenye makubaliano hayo, lakini wanadiplomasia hawaoni mwafaka huo ukidumishwa. Maofisa wa Uingereza, Uchina, Ufaransa, Ujerumani na Urusi wanakutana na naibu waziri wa masuala ya nje wa Iran kuweka mikakati ya kuokoa mwafaka ambao unaelekea kusambaratika.
Rais wa Marekani Donald Trump
"Binafsi pengine sina matumaini, lakini ... najaribu niwezavyo kufikia maamuzi," afisa mwandamizi wa Iran aliwaambia wanahabari kabla ya mazungumzo.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameungana kuhusu mwafaka huo, huku Ubelgiji ikiweka mikakati kuhusu kampuni za Umoja huo kwa kuzingatia vikwazo vya Marekani kwa kuziambia serikali kutuma fedha moja kwa moja katika benko kuu ya Iran ili kuepuka faini.
Afisa huyo amesema kuwa mikakati ya mataifa ya Ulaya itahakikisha kuwa mauzo ya mafuta hayatasitishwa na kwamba Iran itaweza kutumia mfumo wa malipo wa benki ya kimataifa.
Mwafaka wa mpango wa nyuklia unayumbayumba
Marekani haijatisha tu kuiwekea Iran vikwazo lakini pia imetisha kukaza kamba hata zaidi. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo, siku ya Jumatatu alitisha "kuwekea Iran vikwazo vikuu kwenye historia" iwapo haitabadilisha tabia yake kuhusu Mashariki ya Kati.
"Ni kana kwamba Pompeo alikuwa akioga kwenye maji baridi," amesema mwanadiplomasia wa Ulaya. "Tutajaribu kukwamilia mwafaka huo, lakini ...dhana yetu sio mbaya."
Jumatano kiongozi mkuu wa kidini wa Iran alielezea masharti ambayo yatalifanya taifa hilo kusalia kwenye mwafaka huo: hadi Ulaya itoe hakikisho kuwa mauzo ya mafuta ya Iran hayataathiriwa, basi wataendelea na mpango huo.
Aidha alikataa kuwepo kwa mazungumzo mapya kuhusu mpango wa makombora ambao alisema kuwa hayakujumuishwa kwenye mpango wa nyuklia na ambayo Iran inasema kuwa haitasitisha.
Ijumaa afisa huyo wa Iran alisema: "Hatuna muda wa kutosha. Tunatarajia mkutano wa leo kuchukua uamuzi wa pamoja baada ya kujiondoa kwa Marekani."
Mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya
"Kama sio hivyo tutaitisha mkutano wa baraza la mawaziri na kama Iran haitaridhika basi tutachukua uamuzi."
Trump alipuuzilia mbali mwafaka ulioafikiwa na mtangulizi wake Barack Obama, kwa sababu haukujumuisha mpango wa makombora, nafasi yake katika mzozo wa Mashariki ya Kati ama nini kitakachotokea baada ya mwafaka huo kukamilika mwaka 2025.
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa anataka mazungumzo ya mwafaka huo wa nyuklia kukamilishwa miongoni mwa masuala mengine wazo ambalo lilichukuliwa kwa tahadhari kubwa sana na mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin, wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika St. Petersburg siku ya Alhamisi
Maoni