Uholanzi imeiambia Urusi kwamba itaishitaki kwa jukumu lake katika kuangushwa kwa ndege ya Malaysia yenye nambari za safari MH17 tarehe 17 Julai 2014 baada ya uchunguzi kuonyesha kuwa kombora la Urusi ndio lililotumika.
MH17 ilidunguliwa ikiwa katika eneo linalodhibitiwa na waasi wanaoungwa mkono na Urusi mashariki mwa Ukraine wakati ikiwa angani kutoka Amsterdam kuelekea Kuala Lumpur, na kuuwa watu wote 298 waliokuwemo, ambapo karibu theluthi mbili walikuwa raia wa Uholanzi.
Timu ya wachunguzi wa kimataifa ilisema siku ya Alhamisi kuwa mfumo wa makombora wa "Buk" uliotumiwa kuidungua ndege hiyo ya abiria ulitoka kwenye brigade ya 53 ya mashambulizi ya ndege, yenye makao yake katika mji wa Magharibi mwa Urusi wa Kursk.
"Hii ndiyo mara ya kwanza taifa makhsusi kunyooshewa kidole," waziri mkuu wa Uholanzi Mark Rutte aliwaambia waandishi wa habari baada ya mkutano wa dharura wa baraza la mawaziri. "Tunaitwika lawama Urusi kwa ushiriki wao katika kupeleka mfumo wa maroketi wa Buk."
Uhusiano mbaya kabisa kati ya Urusi na Magharibi
Mzozo huo wa kidiplomasia unakuja katika wakati ambapo uhusiano katika mataifa ya Magharibi na Urusi yamefika kiwango chake cha chini kabisaa katika kipindi cha miongo kadhaa.
Mwendesha mashtaka mkuu wa Uholanzi Fred Westerbeke akiwasilisha matokeo ya awali ya uchunguzi unaoedelea kuhusu kuangushwa kwa ndege ya MH17 mwaka 2014.
"Urusi haikutoa ushirikiano kwa maombi ya kisheria ya kimataifa ya kuhusiana na uchunguzi huo," alisema Rutte, akimaanisha uchunguzi uliofanywa na waendesha mashtaka kutoka Australia, Malaysia, Ubelgiji, Ukraine na Uholanzi.
Uholanzi wa Australia ziliiarifu Moscow kwamba wanatarajia Urusi sasa itatoa msaada kamili kwa timu ya uchunguzi, ambayo iko katika hatua yake ya mwisho ya kuwatambua wahusika ili washtakiwe chini ya sheria ya Uholanzi.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Heather Nauert alisema Washington inaunga mkono maamuzi ya Uholanzi na Australia "kuiwajibisha Urusi."
"Ni wakati kwa Urusi kukiri kuhusu jukumu lake katika kuidungua ndege ya MH17 na kuachana na kampeni yake kutoa taarifa za kupotosha," alisema Nauert. Urusi imekanusha wakati wote kushiriki aktika shambulizi hilo, na ilisema siku ya Alhamisi kwamba hakuna kati ya mifumo yake ya ufyatuaji makombora umewahi kuingia nchini Ukraine, licha ya ushahidi wa picha uliowasilishwa na wachunguzi.
Urusi yadai kulengwa katika kampeni ya propaganda
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei Lavrov, alisema siku ya Ijumaa (25 Septemba 2018) kuwa mwenzake wa Uholanzi ameshindwa kutoa ushahidi wa ushiriki wa Urusi katika ajali hiyo, liliripoti shirika la habari la Urusi TASS.
Vipande vya ndege ya Boeing 777 ya shirika la ndege la Malaysia, ambayo ikiwa safarini kama MH17, iliangushwa nchini Ukraine, vikiwa katika ukumbi nchini Uholanzi. Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa kombora la jeshi la Urusi ndiyo lilitumika kuidungua ndege hiyo.
Rutte alikata kutaja hatua zipi hasa zitafuta ikiwa Moscow itaendelea kushindwa kutoa ushirikiano. Spika wa baraza la chini la bunge la Urusi, Vyacheslav Volodin, alinukuliwa na shirika la TASS akisema Ijumaa kuwa Urusi ilikuwa tayari kwa kila kitu, vikiwemo vikwazo vipya.
Urusi tayari imewekewa vikwazo na Marekani na Umoja wa Ulaya kuhusiana na hatua yake ya kuitwaa kimabavu rasi ya Crimea kutoka kwa Ukraine, na kwa hatua yake ya kuyaunga mkono makundi ya waasi wanaopigania kujitenga mashariki mwa Ukraine.
Hivi karibuni zaidi, mataifa kadhaa yaliwafukuza wanadiplomasia wa Urusi kwa mshikamano na Uingereza, ambayo imeituhumu Moscow kwa kutumia sumu ya kuuwa mishipa kumshambulia jasusi wa zamani wa taifa hilo la binti yake katika mji wa Kiingereza wa Salibury mwezi Machi.
Marekani imeimarisha vikwazo mwaka huu baada ya kuituhumu Urusi kwa kuingilia uchaguzi wa rais wa Marekani mwaka 2016. Urusi inasema inalengwa na kampeni ya propaganda
Maoni