Manchester United na Chelsea zote zimo kwenye 10 bora
Manchester United kwa mara nyingine wametangazwa kuwa klabu yenye thamani ya juu zaidi Ulaya, ambapo thamani yao inakadiriwa kuwa €3.25bn (£2.9bn) kwa mujibu wa kampuni ya KPMG.
Klabu hiyo ya England inaongoza kwa "thamani ya biashara", ikiwa mbele ya klabu nyingine kama vile Real Madrid na Barcelona.
Orodha hiyo imeandaliwa baada ya utafiti uliofanywa kwa kuangazia taarifa za kifedha za misimu ya 2015-16 na 2016-17 ambapo waliangazia faida, haki za utangazaji, umaarufu, matarajio kutokana na uwezo wa kimichezo na thamani ya uwanja.
Liverpool, ambao wamefika fainali Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya wamo nafasi ya nane kwenye orodha hiyo.
Kwenye utafiti huo ulioangazia klabu 32 kubwa, klabu za Ligi Kuu ya England zinajaza nafasi sita kati ya 10 za kwanza.
Andrea Sartori, mkuu wa michezo duniani katika KPMG ambaye ndiye mwandishi wa ripoti hiyo, anasema kwa jumla thamani ya klabu za soka imepanda katika mwaka uliopita.
"Ukuaji wa jumla unatokana na sababu kadha, moja ikiwa ni kuongezeka kwa mapato yanayotokana na uendeshaji shughuli katika klabu 32 kuu, ambao ulikuwa ni ukuaji 8%," alisema.
"Uhamisho wa wachezaji wa pesa nyingi pamoja na kuongezeka kwa mishahara hakujazuia klabu kuendelea kuongeza mapato, kwani faida kabla ya kutozwa ushuru uliongezeka kwa mara 17 ukilinganisha na mwaka uliotangulia."
Klabu 10 bora Ulaya kwa 'thamani ya biashara'
Manchester United - €3.255bn
Real Madrid - €2.92bn
Barcelona - €2.78bn
Bayern Munich - €2.55bn
Manchester City - €2.16bn
Arsenal - €2.10bn
Chelsea - €1.76bn
Liverpool - €1.58bn
Juventus - €1.30bn
Tottenham - €1.29bn
Chanzo: KPMG
Kando na kutawala orodha ya 10 bora, kulikuwa na klabu nyingine tatu za Uingereza katika orodha ya 20 bora - West Ham United, Leicester City na Everton.
SSC Napoli (nafasi ya 17) nao wamekuwa klabu ya pili kwa thamani Italia, nyuma ya Juventus lakini mbele ya AC na Inter Milan.
Mwaka huu, klabu 12 zilikuwa na thamani ya zaidi ya euro bilioni moja, mbili zaidi ya 2017 ambapo zilikuwaklabu kumi pekee.
Na klabu sita zina thamani ya zaidi ya euro bilioni mbili, tatu kutoka Ligi ya Premia, mbili kutoka Uhispania na moja ya Ujerumani.
Misimu ya 2015-16 na 2016-17, Manchester United walishinda Kombe la FA, Kombe la Ligi na Europa League. Lakini msimu huu wamemaliza bila kikombe hata kimoja
Maoni