Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na waziri mkuu wa China Li Keqiang wametetea makubaliano ya kinyuklia na Iran, wakati Li akisema kusitisha makubaliano hayo kutaleta utata katika majadiliano na Korea kaskazini.
Merkel na Li walionesha msimamo wa pamoja kuelekea Iran pamoja na biashara huru, masuala mawili ambayo yameshuhudia uingiliaji kati wa Marekani ambapo rais Donald Trump alichukua hatua hiyo. Hayo yalijadiliwa katika mkutano wao katika ziara ya kansela Merkel mjini Beijing.
waziri mkuu wa China Li Keqiang (kushoto) akizungumza na kansela wa Ujerumani Angela Merkel (kulia)
Li alionya kwamba kusitisha makubaliano hayo na Iran, hakutaiathiri tu Iran, lakini pia kutakuwa na athari hasi katika uwezo wa kutatua masuala mengine mazito kupitia majadiliano ya amani.
Hakuitaja Korea kaskazini kwa jina , lakini wachambuzi wameonya kwamba kujitoa kwa Trump kutoka katika makubaliano hayo na Iran kunachafua uaminifu wa Marekani kabla ya mkutano uliopangwa kufanyika katika ya kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un na Trump mwezi ujao.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel pia alieleza wasi wasi wake juu ya athari za kiuchumi kwa Ulaya kutokana na hatua hiyo ya Trump kujitoa kutoka katika makubaliano na Iran.
Uamuzi wa Trump kurejesha vikwazo dhidi ya Iran , licha ya maombi kutoka kwa washirika kuendelea na makubaliano hayo, kunaweza kuathiri makampuni ya ulaya ambayo yanafanya biashara nchini Iran tangu yaliposainiwa makubaliano hayo mwaka 2015.
Kansela Merkel akisimama karibu na treni yendayo kasi iliyotengenezwa na kampuni ya Ujerumani nchini China.
Makampuni ya Ulaya
Iwapo makampuni ya Ulaya yatajitoa ama kupunguza operesheni zao nchini Iran kwa kuhofia vikwazo vya marekani , hali hiyo italeta fursa kwa makampuni kutoka mataifa mengine kuingia nchini Iran na kufanyabiashara ," Merkel alisema.
kuhusiana na biashara , Merkel alikaribisha hatua ya China ya kupunguza ushuru kwa magari yanayoingia nchini humo na kuruhusu makampuni ya magari ya kigeni kumiliki hisa kubwa katika miradi ya pamoja na washirika wao wa China.
Kansela amezungumzia pia madai ya Ujerumani kwa China ya kupunguza vizuwizi katika uwekezaji wa nje , akisema nchi hizo mbili zitatia saini makubaliano ya kuwezesha kila nchi kupata fursa ya kuingia katika soko la mwenzake kwa upande wa magari.
Waziri mkuu wa China Li Keqiang
"China na Ujerumani zimo katika njia ya kuhimiza mahusiano na mataifa mengine pamoja na kuimarisha biashara huru," alisema Merkel , ambaye aliongozana na ujumbe wa viongozi wa makampuni 18 kutoka Ujerumani.
Li alidokeza kwamba makubaliano ya uwekezaji kati ya China na Umoja wa Ulaya, ambayo yamekuwa yakifanyiwa kazi kwa muda mrefu, huenda yakatiwa saini wakati wa mkutano wa pande hizo mbili wa kila mwaka mwezi Julai mjini Beijing
Maoni