MTEULE THE BEST
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa Makubaliano ya Paris juu ya mabadiliko ya tabia nchi yataanza kutekelezwa kuanzia tarehe 4 Novemba.
Makubaliano hayo yataanza kutekelezwa siku 30 baada kuidhinishwa na zaidi ya nchi 55 zinazozalisha takribani zaidi ya asilimia 55 ya hewa chafuzi duniani.
Juzi Jumatano Umoja wa Mataifa ulisema kuwa pande 73 za makubaliano hayo zinazozalisha asimilia 56.87 tayari zimeidhinisha makubaliano hayo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametoa taarifa iliyosema kuwa uungwaji mkono wa nguvu wa makubaliano hayo ya Paris kutoka kwenye jumuia ya kimataifa ni uthibitisho wa hitaji la haraka la uchukuaji hatua.
Mataifa mawili yanayoongoza kwa uzalishaji wa hewa chafuzi duniani China na Marekani yaliidhinisha makubaliano hayo mwezi uliopita na kusababisha nchi nyingine saba wanachama wa Umoja wa Ulaya kuharakisha mchakato wao wa kuidhinisha makubaliano hayo.
Makubaliano hayo yataanza kutekelezwa kabla ya kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi litakalofanyika Morocco mwezi Novemba mwaka huu. Mkutano wa kwanza wa utiaji saini makubaliano hayo utafanyika pembezoni mwa kongamano hilo.
Rais wa Marekani Barack Obama amepokea tangazo la Umoja wa Mataifa na kusema imekua ni siku ya kihistoria kwenye mapambano ya kuilinda dunia kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Maoni