MTEULE THE BEST
Wengi tunajua kuwa alikuwa mhehe, ila leo nawaletea makala hii yenye kuchokoza mjadala juu ya Asili ya Chief Mkwawa.
……………………………………
Mtwa Mkwawa hakuwa Mhehe na wala hakuwa mtoto wa Mnyigumba (kama historia iliyoandikwa na Wajerumani na inapotosha); bali Mkwawa alikuwa ni mtoto wa dada yake Mnyigumba ambaye aliolewa na Mtemi wa Waluguru. Hivyo Mkwawa alikuwa Mluguru kwa asili.
Akiwa mdogo alikwenda kumtembelea mjomba wake (Mnyigumba) na kutokana na ushujaa wake, Mkwawa alishiriki kupiga vita vikali dhidi ya Wangoni pale Makambako. Mnyigumba akampenda Mkwawa kuliko watoto wake, na ndio chanzo cha kupewa urithi pamoja na mtoto wa Mnyigumba aliyeitwa Muhenga. Ndio maana Muhenga (mtoto orijino wa Munyigumba), akawa na bifu kali na Mkwawa na bifu hilo halikuisha hadi Muhenga alipofariki!
Sherehe za kuapishwa Mtwa Mkwawa zilifanyika Dodoma eneo la Mpwapwa. Sherehe hizo zilihudhuriwa na wajomba zake—Mtemi Mazengo, Kimweri, Lugulu na Mirambo. Inasemekana wakiwa katika kushangilia na kuimba, “Mpwa! Mpwa!” na ndipo neno Mpwapwa likazaliwa.
Mtwa Mkwawa alikuwa na vikosi vinne vya jeshi la vita; kimojawapo kilikuwa cha upelelezi na ushambuliaji (Kiitwacho Vamalavanu) ambacho kilikuwa kikila nyama ya mbwa ikichanganywa na dawa ya tambiko. Wahehe waliamini kuwa watakuwa na uwezo wa kunusa maadui na wao kutoonekana. Hivi ndivyo ulaji nyama ya mbwa ulivyoanza huko Uheheni na sharti ilikuwa kwamba mchuzi wa mbwa unywewe ukingali wa moto!
Mtwa Mkwawa alijua kusoma na kuandika kwa ufasaha lugha ya Kiarabu na alikuwa muumini wa dini ya Kiislamu. Mambo yalipokuwa magumu, Mtwa Mkwawa aliandika barua ya kwenda kwa Wajerumani akiwaomba wampe (upenyo) wa kuwashambulia makabila ya Wabena na Wakinga ambao walijisalimisha na kupatana na Wajerumani.
Watafiti tunajiridhisha kwamba hii ilikuwa ishara ya Mtwa Mkwawa kukata tama, maana isingekuwa rahisi kwa Wajerumani kumruhusu kufanya alichotaka.
Mtwa Mkwawa hakujipiga risasi, bali alijitumbukiza katika daraja la Kikongoma lililopo Mto Ruaha—mahali ambapo mama yake mzazi pia alijitumbukiza na kujiua pale. Lile fuvu linalodaiwa kuwa ni la Mtwa Mkwawa, halikuwa lake ila inadaiwa kwamba ni fuvu la mlinzi wake. Hadi leo hakujawahi kufanyika DNA na kuthibitisha fuvu hilo.
Kwenye vita iliyomsambaratisha Mtwa Mkwawa, Wajerumani walifanikiwa kumkamata mdogo wake aliyeitwa Mpangile. Walimtundika kitanzini lakini hakufa, wakampiga risasi, hakufa! Baadae akatoboa siri kuwa wammwagie maji na wamchome mkuki-ndipo atakufa!
Baada ya kuona hivyo Wajerumani wakampa jina “Mpangelwangindo Mgopisala Sasisinagopi”ikiwa na maana ya Mpangile anaeogopa mkuki risasi haogopi. Hapo walipomuulia Mpangile panaitwa Kitanzini mpaka leo!
Kutokana na kuwa Mluguru kwa asili, ndio maana Mtwa Mkwawa alikuwa na uhusiano wa karibu na Mtemi Mazengo (Ugogo Dodoma), pamoja na Mtemi Mirambo wa Unyamwezini Tabora. Mazengo, Mirambo na Mtemi wa Uluguru, walikuwa ndugu wa damu na walikuwa wajomba wa Mkwawa. Tunaambiwa hata wakati wa kurejesha fuvu linalodaiwa kuwa la Mtwa Mkwawa kutoka Ujerumani, na kuliweka kwenye Makumbusho ya Mkwawa pale Kalenga, Wagogo walimiminika kutoka Dodoma kwa wingi sana na walikuwa wakiimba na kucheza kwa bidii na kwa nguvu kupita hata Wahehe wenyewe!
Mtwa Mkwawa alikuwa na rada za asili alizozitega milimani ambazo zilikuwa zikimjulisha hali ya vita na ujio wa maadui katika himaya yake. Rada hizo zilizoitwa “Vimwanyula”, zilipoangushwa na Wajerumani ndio ulikuwa mwanzo wa kushindwa kwa Mtwa Mkwawa katika vita. Siku Vimwanyula vilipoanguka kwa mashambulizi ya Wajerumani, Wahehe walilia hivi: “Fimwanyula figwe, Ililinga lyavembile danda” wakimaanisha; “Rada zimeanguka na sasa Iringa inalia machozi ya damu”
Mkuu wa Kikosi cha Usalama wa Ufalme wa Mtwa Mkwawa aliyeitwa Chavala, ndie aliesababisha anguko la Mkwawa mbele ya Wajerumani baada ya kuanika siri zote za kijeshi, kimizimu na kiganga alizokuwa akitumia Mkwawa. Chavala alishawishika kumuasi Mkwawa baada ya kupewa rupia 5,000 na Wajerumani.
Mtwa Mkwawa alikuwa na zake 63, waliokuwa wakiishi Ipamba na mamia ya watoto aliowajengea makazi eneo la Tosamaganga. Kwa sasa Ipamba pamejengwa Hospitali na Tosamaganga kuna shule na misheni.
Historia inayofundishwa shuleni na vyuoni kuhusu Mtwa Mkwawa na ambayo iliandikwa na wakoloni, imepindishwa sana. Wajerumani walikipata cha mtema kuni na kwa jeuri na kwa makusudi, hawajaingiza matendo na mambo mengi sana ya kishujaa aliyofanya Mtwa Mkwawa.
Mathalani, kwenye historia, Wajerumani wanasema askari wao waliouawa na jeshi la Mkwawa pale Lugalo, walikuwa mia tatu (300), lakini wazee walinieleza kwamba askari wa Kijerumani waliofariki pale walikuwa zaidi ya elfu tano!
Naamini umepata japo kitu na itakuamsha kuwa mtafiti kwa mambo unayofundishwa ama kuambiwa ama kusoma.
Mie najiuliza, ikiwa historia inayotuzunguka kama ya Mtwa Mkwawa wameipindisha namna hii, je, hayo masomo mengine kuna pumba ngapi zimeingizwa humo? Maana masomo mengi na mitaala yetu shuleni na vyuoni tumeikopi na kupesti kutoka kwao! Nina wasiwasi, mfumo wa elimu yetu unazalisha wasomi vibogoyo ambao, badala ya kutawala mazingira, wananyanyaswa na mazingira.
Makala hii imeandaliwa na Ndugu, Albert Nyaluke Sanga.
Kama una ushaidi juu ya asili ya Mkwawa wa Uhehe, tuwasiliane! Ni wakati wa kuandika historia yetu na kuacha historia iliyopindishwa na wakoloni na vijibwa vyao.
Maoni