Walevi waunda kisiwa New Zealand kukwepa marufuku
MTEULE THE BEST
Watu hao waliunda kisiwa kwa kutumia mchanga katika juhudi za kukwepa marufuku
Wakazi kadha wa New Zealand walitumia ubunifu wa hali ya juu katika kinachoonekana kuwa juhudi za kukwepa marufuku ya kunywa pombe maeneo ya umma.
Maji yalipokupwa baharini, walitumia mchanga kuunda 'kisiwa' kidogo katika sehemu ambayo mto Tairua unamwaga maji yake baharini katika rasi ya Coromandel Jumapili alasiri.
Kisha, waliiweka meza yao ya safari na kufungua chupa zao za vinywaji na kuanza kujiburudisha.
Wakazi walifanya mzaha kwamba walikuwa kwenye "eneo la bahari la kimataifa" lisilomilikiwa na taifa lolote hivyo hawangeathirika na marufuku hiyo ya pombe.
Watu hao walibugia vinywaji vyao hadi usiku mkesha wa Mwaka Mpya na kutazama fataki zikirushwa kuukaribisha mwaka mpya kwa mujibu wa tovuti ya New Zealand ya stuff.co.nz.
Kisiwa chao bado kilionekana Jumatatu asubuhi.
Marufuku dhidi ya unywaji pombe hadharani ilitangazwa Coromandel kipindi cha mwaka mpya na waliokiuka marufuku hiyo walikabiliwa na faini ya $250 (£130; US$180) au kutiwa mbaroni.
Lakini maafisa wa serikali wanaonekana kuchukuliwa kisa cha kundi hilo la watu kwa ucheshi.
"Huo ni ubunifu wa hali ya juu - laiti ningelijua kuhusu hilo pengine ningejiunga nao," kamanda wa polisi wa eneo hilo Inspekta John Kelly alisema alipofahamishwa kuhusu kisiwa hicho.
Kisiwa hicho bado kilionekana asubuhi Januari mosi
Picha zao zilipakiwa kwenye kundi la wakazi kwenye Facebook la Tairua ChitChat na David Saunders.
Aliambia BBC kwamba inafurahisha kuwa kuna wakazi walioamua kujiburudisha.
Lakini mwanaharakati mwingine Noddy Watts alisema marufuku hiyo haijafanikiwa na badala yake watu wengi wamekamatwa.
Amesema polisi sana wanakabiliana na vijana walevi.
"Hiyo siyo kazi yao, hiyo ni kazi ya wazazi," alisema kwa mujibu wa gazeti la New Zealand Herald.
Maoni