Baada ya juma zima la kuwepo kwa hofu ya kutoweka kiasi cha shilingi trilioni 1.5 za Kitanzania serikalini, hatimaye leo serikali ya Rais John Magufuli imetoa ufafanuzi bungeni juu ya wapi kilipo kiasi hicho cha fedha.
Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli.
Baada ya juma zima la kuwepo kwa hofu ya kutoweka kiasi cha shilingi trilioni 1.5 za Kitanzania katika mazingira ya kutatanisha katika makadirio ya bajeti ya serikali ya Tanzania, hatimaye leo serikali ya Rais John Magufuli imetoa ufafanuzi bungeni juu ya wapi kilipo kiasi hicho cha fedha.
Ufafanuzi huu unatolewa baada ya kuwepo kwa kile kilichoonekana kama ukosoaji wa wazi na wasiwasi juu ya matumizi mabaya ya fedha za umma na yasiozingatia sheria kutoka kwa viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani na hata wananchi wa kawaida kwa takribani juma zima.
Akitoa mchanganuo wake, Naibu Waziri huyo wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji amesema kiasi cha shilingi bilioni 697 kilitumika kwa matumizi ya dhamana na hati fungani zilizoiva. Na kingine bilioni 687 kilikuwa kwa ajili ya mapato tarajiwa.
Fungu la fedha kwa ajili ya Zanzibar
Rais John Magufuli na Rais wa Zanzibar Ali Mohammed Shein
Aidha naibu waziri aliongeza kusema kiasi shilingi bilioni 203 kilikusanywa kama kodi kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Amesema kutoonekana kwa fedha hizo kunatokana na taarifa ya ukaguzi wa Mkaguzi wa Mdhibiti wa Hesabu za Serikali CAG kutumia nyaraka za hesabu mbalimbali, na hivyo kutojumuisha taarifa za utekelezaji wa bajeti, akiongeza kuwa hadi Juni mwaka 2017 mapato yalifikia shilingi trilioni 25.3. na matumizi kufikia trilioni 23.79.
Ukosoaji wa serikali unaendelea
Hata hivyo, tayari ufafanuzi huu wa serikali juu ya zilipo shilingi trilioni 1.5 umeanza kukosolewa vikali. Msemaji wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, ambaye chama chake ndicho kilichoanzisha udadisi wa matumizi ya fedha hizo, ameiambia DW kwa njia ya simu kuwa bado serikali haijasema ukweli na kwamba wanajiandaa kueleza upungufu uliojitokeza.
Itakumbukwa hivi karibuni nchini humo, baada ya taarifa ya mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali kuwekwa hadharani kiongozi wa chama cha siasa cha upinzani cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, alijitokeza hadharani kusema fedha hizo hazikutolewa kwa matumizi kwa hivyo hazikukaguliwa, na hivyo kuzusha mjadala unaoendelea hadi wakati huu.
Sakata hili la shilingi trilioni 1.5 ni la kwanza la aina yake kwenye taifa hilo kubwa la Afrika Mashariki na wengi wanalichukulia kuwa ni suto kwa utawala wa miaka miwili wa Rais Magufuli, ambaye amejijengea sifa ya kupambana na ufisadi, ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma
Maoni