Korea Kaskazini imetangaza kusitisha mara moja majaribio yote ya silaha za nyuklia na makombora ili kujikita katika kusaka maendeleo ya kiuchimi na amani kwenye rasi ya Korea.Imetangaza pia kufunga kituo cha majaribio.
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amesema nchi yake haihitaji tena kufanya majaribio ya makombora ya masafa marefu kwa sababu imekamilisha lengo lake la kutengeneza silaha za nyuklia, limeripoti shirika la habari la nchi hiyo KCNA.
Korea Kaskazini imesema ili kuunda mazingira ya kimataifa yenye kufaa kwa uchumi wake, itawezesha mawasiliano ya karibu na mjadala pamoja na mataifa jirani na jumuiya ya kimataifa.
Hii ni mara ya kwanza kwa Korea Kaskazini kuzungumzia moja kwa moja mpango wake wa silaha za nyuklia, na imekuja siku kadhaa kabla ya mkutano wa kilele unaoandaliwa kati ya Kim na rais wa Korea Kusini Moon Jae-in wiki ijayo, na mkutano na rais wa Marekani Donald Trump mwishoni mwa mwezi Mei au mwanzoni mwa Juni.
"Uwanja wa kaskazini wa majaribio ya nyuklia wa DPRK (Jamhuri ya Watu wa Korea Kaskazini) itavunjwa kuhakikisha kwa uwazi, usitishaji wa majaribio ya nyuklia," ilisema KCNA baada ya kim kuitisha mkutano wa kamati kuu ya chama tawala cha Wafanyakazi siku ya Ijumaa.
"Tutaelekeza juhudi zote kwenye kujenga chumi ya kisoshalisti yenye nguvu, na kuboresha viwango vya maisha ya watu kupitia uhamaishaji wa raslimali zote za watu na nyenzo za taifa," lilisema KCNA.
Picha hii iliopigwa Aprili 15, 2017 inaonyesha roketi ambalo halikutambuliwa, linaliripotiwa kuwa aina ya Hwasong, wakati wa gwaride la kijeshi mjini Pyongyang.
Trump: Maendeleo kwa wote
Trump alikaribisha taarifa hiyo ya Kim na kusema anausubiri kwa hamu kubwa mkutano kati yake na Kim. "Korea Kaskazini imekubali kusitisha majaribio yote ya nyuklia na kufunga vituo vikuu vya kufanyia majaribio. Hii ni habari njema kwa Korea Kaskazini na ulimwengu - Hatua kubwa! Nina shauku juu ya mkutano wetu," Trump alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter.
Katika ujumbe mwingine wa Twitter, Trump alisema: "Ujumbe kutoka kwa Kim Jong Un: 'Korea Kaskazini itasitisha majaribio ya nyuklia na ufyatuaji wa makombora ya masafa marefu.' Pia itafunga kituo cha majaribio ya nyuklia kaskazini mwa nchi kudhihirisha azma ya kusitisha majaribio ya nyuklia."
Lakini tangazo la Korea Kaskazini halikusema bayana iwapo Pyongyang ina nia ya kuachana kabisaa na silaha za nyuklia au kupunguza utengenezaji wa makombora na vipuri vyake. Sera mpya ya Korea Kaskazini inaweka mazingira ya majadiliano zaidi wakati mkutano wa kilele utakapofanyika.
Korea Kusini ilisema uamuzi huo wa Kaskazini uliashiria hatua za maana kuelekea uondoaji wa silaha za nyuklia katika rasi ya Korea na yataweka mazingira yanayofaa kwa mikutano yenye ufanisi na Seoul na Marekani.
Japan yakaribisha tangazao kwa tahadhari
Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe alisema anaikaribisha taarifa ya Korea Kaskazini, lakini inapaswa kupelekea kuwepo na uondoaji wa nyuklia unaoweza kuthibitika.
"Tangazo hilo ni hatua nzuri ambayo napenda kupongeza," Abe aliwaambia waandishi habari. "Lakini kilicho muhimu ni kwamba hilo linepelekea uondoaji kamili na unaothibitika wa nyuklia. Nataka kusisitiza hili."
Watu wakiangalia luninga inayoonyesha picha za kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, kulia, rais wa Korea Kusini Moon Jae-in, katikati, na rais wa Marekani Donald Trump, katika kituo cha treni cha Seoul, Machi 7, 2018.
Waziri wa ulinzi wa Japan Itsunori Onodera alisema awali kwamba Japan "haiwezi kuridhishwa", kwa sababu Pyongyang haikuzungumzia kuachana na mpango wake wa makombora ya masafa ya kati na marefu.
Onondera alisema Tokyo itaendeleza sera yake ya kuiwekea mbinyo hadi hapo itakapoachana na "silaha za mangamizi ya watu wengi, silaha za nyuklia na makombora."
Hofu ya vita
Kora Kaskazini imetetea programu zake za nyuklia na makombora kama kizuwizi muhimu dhidi ya uhasama wa Marekani. Imefanya majaribio mbalimbali ya makombora, na mwaka uliopita iliripua bomu lake lenye nguvu zaidi la nyuklia.
Majaribio hayo na majibizano makali kati ya Trump na Kim vilisabisha hofu ya kuzuka kwa vita hadi kiongozi wa Korea Kaskazini katika hotuba ya mwaka mpya, alipotoa wito wa kupunguza mzozo wa kijeshi. Baadae aliboresha uhusiano na Korea Kusini na kutuma ujumbe katika michezo ya olimpiki ya majira ya baridi iliyofanyika Korea Kusini mwezi Februari.
Nam Sung-wook, profesa wa masomo ya Korea Kaskazini katika chuo kikuu cha Korea mjini Seoul, alisema inaweza kuchukuliwa kama kioja kwamba Kim Jong Un mwenyewe ndiyo ametangaza mipango ya kusistisha uendelezaji wa nyuklia, lakini aliongeza kuwa matamshi hayo ya kiongozi wa Korea Kaskazini yameacha maswali kadhaa.
"Bado haijawa wazi iwapo inamaanisha kwamba Kaskazini haitaendelea tu na uendelezaji wa programu zake za nyuklia katika siku za usoni, au iwapo watafunga kabisaa vituo vyote vya nyuklia. Na ni watazifanyia silaha za nyuklia zilizopo kwa sasa?" Nam alisema.
Kim Jong Un akisherehekea kilichoelezwa kuwa ufyatuaji wa kombora la masafa ya kati chapa ya Hwasong-12 katika eneo lisilotajwa Korea Kaskazini. Picha hii ilisambazwa Septemba 16, 2017.
Shinikizo kuendelea dhidi ya Pyangyang
Korea Kaskazini imeeleza dhamira yake kwa "uondoaji kamili wa nyuklia" katika rasi ya Korea na haijaambatanisha mashrti yoyote, alisema rais wa Korea Kusini Moon Jae-in siku ya Alhamisi, lakini Washington imeendelea kuwa na wasiwasi na iliapa kuendeleza shinikizo dhidi ya Pyongyang.
Marekani ilisema Alhamisi kwamba wakati maandalizi yakifanyika kwa ajili ya mkutano kati ya Trump na Kim, mataifa yanapaswa kuendelea kuiwekea Pyongyang shinikizo la kifedha na kidiplomasia, ili kusalimisha silaha za nyuklia zilizopigwa marufuku.
Vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini, vilivyowekwa baada ya jaribio lake la kwanza la nyuklia mwaka 2006, na kurefushwa katika kipindi cha muongo mmoja, vinalenga kuinyima Korea Kaskazini kiwango kikubwa cha biashara ya kimataifa.
Mkutano wa kamati kuu ya chama tawala cha Korea Kaskazini uliofanyika Ijumaa uliitishwa kujadili "masuala ya kisera ya hatua mpya" ili kukidhi matakwa ya "kipindi muhimu cha sasa cha kihistoria," lilisema shirika la habari la KCNA.
Maoni