MTEULE THE BEST
Korea Kaskazini imefyatua kombora la masafa marefu kupitia anga ya kisiwa cha Hokkaido nchini Japan.
Jeshi la Korea Kusini linasema kuwa kombora hilo limefyatuliwa kutoka maeneo ya karibu na mji mkuu wa Pyongyang.
Mwandishi wa BBC mjini Tokyo anasema kuwa kombora hilo lilipita anga za juu zaidi na kwenda mbali zaidi ikilinganishwa na kombora la awali.
Jaribio hilo linakuja siku chache tu baada ya baraza la Usalama la Umoja wa mataifa kuidhinisha vikwazo zaidi dhidi ya Korea Kaskazini.
Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa marekani Rex Tillerson ametoa wito kwa China na Urusi kuchukuwa hatua za moja kwa moja dhidi ya Pyongyang, huku waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe akitaja jaribio hilo la hivi punde kuwa ni kitendo cha kuudhi.
"China huiuzia Korea kaskazini mafuta yake huku Urusi likiwa ndio taifa lililowaajiri raia wengi wa Korea kaskazini.
China na Urusi lazima zionyeshe kwamba zimechoshwa na hatua ya Korea Kaskazini kuendelea kufanyia majaribio makombora yake kwa kuichukulia hatua ya moja kwa moja.
Dakika chache baada ya ufyatuzi huo Korea Kusini ilifyatua makombora mawili ya masafa marefu baharini katika hatua ya kuionya Korea Kaskazini kulingana na chombo cha habari cha Yonhap.
Rais Moon Jae-in alifanya kikao cha dharura na kuonya kwamba kombora hilo litasababisha vikwazo zaidi dhidi ya Korea kaskazini.
Jeshi la Korea Kusini limesema kuwa jaribio hilo la hivi karibuni ,likiwa la kwanza tangu vikwazo dhidi ya Korea kaskazini kuimarishwa wiki iliopita lilifanyika katika eneo la Sunan Kaskazini mwa Pyongyang.
Na kama kombora la hapo awali, hili la sasa pia lilipitia katika anga ya kisiwa cha Japan kilichopo kaskazini mwa taifa hilo cha Hokkaido na kuanguka katika bahari ya pacific.
Ving'ora vililia katika eneo hilo vikitoa tahadhari kwa raia kujificha.
Kulingana na makadirio ya awali, kombora hilo lilirushwa juu zaidi ya lile lililorushwa mnamo Agosti tarehe 29 ambalo Pyongyang ilionya ni operesheni yake ya kwanza ya kijeshi katika eneo la Pacific.
Waangalizi wanasema kuwa kombora hilo ni la masafa ya wastani , ijapokuwa maafisa wa Japan wanasema kuwa kuna uwezekano mkubwa kwamba ni kombora la masafa marefu linaloweza kurushwa kutoka bara moja hadi jingine ICBM.
Eneo la Guam linalomilikiwa na Marekani katika bahari ya Pacific ambalo Korea Kaskazini imeonya kulishambulia liko kilomita 3,400 kutoka Pyongyang hivyobasi linaweza kufikiwa na kombora hilo.
Maoni