MTEULE THE BEST
Tanzania imesema imeshtushwa baada ya kuorodheshwa miongoni mwa nchi ambazo zimechunguzwa na Umoja wa Mataifa na kuhusishwa kuwa na uhusiano wa kibiashara na Korea Kaskazini.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, waziri wa mambo ya nje Dkt. Augustine Mahiga, amesema licha ya uhusiano uliokuwepo awali, lakini tangu mnamo mwaka 2014, Tanzania imepunguza kabisa uhusiano wa kibiashara na kidiplomasia na nchi hiyo.
"Hatuna ugomvi na Korea Kaskazini,lakini kitendo chao cha kutengeneza masilaha ya kuangamiza sio mazuri kwa heshima na usalama duniani.Ndiyo maana tukaanza kuchukua hizo hatua za kupunguza mahusiano." amesema Dr Mahiga kwa waandishi wa habari leo.
Waziri Mahiga ameongeza kusema kuwa, uhusiano huo wa kibiashara ulikuwepo kabla ya vikwazo vilivyowekwa hivi karibuni na Baraza la Umoja wa Mataifa.
Waziri huyo amesema anaelekea katika mkutano wa kawaida wa Umoja wa Mataifa, ambapo atatumia fursa hiyo kujibu tuhuma hizo kwa Baraza la Usalama.
Tanzania na Uganda ni miongoni mwa baadhi ya nchi zinazochunguzwa na Umoja wa Matiafa kwa tuhuma za kwenda kinyume na vikwazo vilivyowekwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini.
Ripoti ya uchunguzi huo ilitolewa mnamo tarehe 9 mwezi wa Septemba. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesema linachunguza tuhuma za Tanzania kuingia mikataba ya kijeshi na Korea Kaskazini inayogharimu dola za kimarekani milioni 12.5.
Maoni