Tanzania yatia saini ujenzi wa mradi wa umeme unaopigiwa kelele na wanamazingira, Rais Magufuli asema ni mradi wa lazima kwa maendeleo
Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
Rais wa Tanzania John Magufuli amesema kutekelezwa kwa mradi mkubwa wa uzalishaji umeme wa Stigler's Gorge ni jambo la lazima.
Leo rais wa nchi hiyo John Magufuli ameweka saini na wakandarasi wa mradi huo kutoka Misri wakiwa pamoja na waziri mkuu wa nchi yao.
Hatua hiyo inakuja baada ya miaka 40 tangu utafiti wa uzalishaji wa umeme kutoka mto Rufiji ambao unaweza kuzalisha megawati 2,100 kufanyika wakati huo Tanzania ikiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere.
Mradi huu unatarajiwa kutekelezwa na fedha za watanzania wenyewe kwa kiwango cha dola za kimarekani bilioni 2.9 ambayo ni sawa na takribani shilingi trilion 6.5 za kitanzania.
Na kampuni itakayofanya kazi hiyo inatoka Misri.
Rais Magufuli amesema kwamba walitumia muda kutafakari kuhusu mradi huu kwa sababu Tanzania imebarikiwa na vyanzo vingi sana vya uzalishaji umeme kama vile maji,gesi asilia,upepo,joto ardhi ,makaa ya mawe pamoja na madini ya urani. Na kufikia uamuzi huo waliangalia vigezo vikubwa vinne ambavyo ni:
Uhakika wa chanzo
Gharama za utekelezaji
Uzalishaji wa umeme
Tija au manufaa yanayotarajiwa
Na mwisho kuligundua kuwa mradi wa maji ya Rufiji ndio unaifaa zaidi kwa Tanzania kwa muda huu.
Sababu chanzo chake ni cha uhakika na maji yake yanatoka katika mito inayotoa wastani wa mvua.
Vilevile kuna uwezo wa kuzalisha umeme kwa zaidi ya miaka 60 ijayo .
"Mradi huu utatumia fedha kidogo kuliko vyanzo vingine vya umeme, Uniti moja inayozalishwa na umeme wa maji ni shilingi 36 na huku umeme unaotengenezwa na nyukilia ni shilingi 65 kwa uniti moja wakati umeme wa jua ni shilingi 103.05 , upepo ni shilingi 103.05, makaa ya mawe ni shilingi 118, Gesi asilia shilingi 147 na mafuta shilingi 426 kwa uniti moja. Hivyo utofauti ni mkubwa sana kati ya maji na vyanzo vingine" Rais Magufuli alieleza.
Hata hivyo, mradi huo umekuwa ukipingwa vikali na wanaharakati na mashirika ya mazingira ndani na nje ya Tanzania. Wanasema ujenzi huu unaweza kuleta madhara makubwa kwa viumbe hai pamoja na binadamu wanaoishi katika eneo hilo.
Mfuko wa Mazingira wa Kimataifa (WWF) umeshatoa ripoti inayoonyesha madhara ya kimazingira na uhifadhi wa mradi huo.
"Kuna matokeo makubwa zaidi ya mafuriko ya kilometa za mraba 1,200 za eneo linalohitajika na ujenzi wa bwawa hilo. Kutakuwa na ongezeko la mmomonyoko wa ardhi utakaosababisha kukauka kwa vyanzo vya maji yanayotegemewa na wanyamapori, hivyo kuathiri sekta ya utalii.
"Itapunguza rutuba katika ardhi na mazingira ya delta ya Rufiji na upatikanaji wa samaki aina ya kamba kochi na samaki wengineo wanaopatikana katika eneo hilo na hivyo kuathiri maisha ya wananchi wapatao 200,000 wanaoishi maeneo hayo," imesema ripoti hiyo.
Hata hivyo rais Magufuli leo amesisitiza kuwa mradi huu wa umeme utaleta manufaa makubwa kwa nchi hiyo tofauti na madai ya baadhi ya watu wanaodai kuwa mradi utaharibu mazingira.
"Umeme wa maji ni rafiki wa mazingira na utapunguza ukataji wa miti na kutunza mazingira yetu na itaokoa miti inayokatwa kwa ajili ya kuni na mkaa kwa watu kutumia umeme...Tani milioni 2.3 za mkaa kwa mwaka zitatumia miti milioni 30 hivyo basi uwepo wa mradi huu utasaidia kupunguza ukataji wa miti.Hivi sasa kila siku kunavunwa hekta 583 ya miti kwa mwaka, eneo la selou lina ukubwa wa hekta mil.5 hivyo kwa ukataji huu wa miti baada ya miaka kumi na tano tu, selou inaweza kupotea.
"Mradi huu ni muhimu sana kutunza mazingira ya nchi yetu hivyo basi wapenda mazingira wote inabidi waunge mkono jambo hili. Uwepo wa umeme wa uhakika utasaidia watu wasikate miti na kutumia umeme."
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na Balozi wa Misri Tanzania, Mohamed Gaber Mohamed Abulwafa
Utofauti wa gharama za umeme katika mataifa mengine
Kwa sasa Tanzania inalipa dola za marekani senti 10.7 kwa uniti kiasi ambacho ni kikubwaa tofauti na nchi nyingine huku Misri ni senti 4.6$ , korea ya kusini na china ni ya cent 8$, Afrika kusini senti 7.4$, India senti 6.8$ , Ethiopia senti 2.4$, Uingereza senti 0.15$, Marekani senti 0.12 $.
Hali ambayo inapelekea kuwepo kwa gharama kubwa kwa bidhaa za Tanzania kuwa tofauti na nyingine kutokana na gharama ya umeme.
Mradi huu unakadiriwa kukamilika baada ya miaka mitatu na nusu huku 15% ya malipo ikiwa ipo tayari kulipwa kama kianzio cha mradi
Maoni