John Bolton amepewa jukumu la kupanga jinsi ya kuniangamiza'
Rais wa Venezuela Nicolas Maduro akizungumza na wanahabari mjini Caracas Desmba 12,2018
Rais wa Venezuela Nicolás Maduro amedai kuwa Marekani inapanga njama ya kumuua na kupindua serikali yake.
Amewaambia wanahabari kuwa mshauri wa usalama wa kitaifa wa Marekani John Bolton, anahusuka moja kwa moja na njama hiyo japo hakutoa ushahidi wowote kuthibitisha madai hayo.
Rais Trump amemtaja Maduro kama kiongozi wa kiimla na kumwekea vikwazo.
Mapema wiki hii maafisa wakuu wa Urusi na Marekani walijibizana baada ya ndege mbili kubwa za kuangusha mabomu za Urusi kutua nchini Venezuela, taifa linalopatikana Amerika Kusini.
Ndege hizo za kivita aina ya Tu-160 zilitua Venezuela Jumatatu katika kile kinachoonekana kama jaribio la kuonyesha uungaji mkono wa Urusi kwa rais wa kisoshialisti wa Venezuela Nicolás Maduro ambaye amekuwa akikabiliwa na shinikizo.
Ndege hizo mbili zina uwezo wa kubeba silaha za nyuklia.
Maduro alisema nini?
"John Bolton amepewa jukumu la kupanga namna ya kuniangamiza, kuleta vikosi vya kigeni na kubuni serikali ya mpito nchini Venezuela," aliwaambia wanahabari katika ikulu ya rais ya Miraflores.
Watu wa Venezuela wanajiandaa kukabiliana na hatua hiyo kwa usaidizi wa "mataifa rafiki zake," alisema,
Bwana Maduro aliwahi kuituhumu Marekani, Colombia na upinzani kwa kupanga njama ya kumuua.
Ni yapi yaliyomo katika ziara ya walipuaji wa mabomo wa Urusi?
Marekani imekuwa ikikwazika na uhusiano wa karibu wa serikali ya Maduro na Urusi, Uchina na mataifa mengine ambayo yanatofautiana na utawala wa Trump.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amesema kitendo hicho ni sawa na "serikali mbili fisadi kufuja mali ya umma."
Waziri wa Ulinzi Vladimir Padrino (mshororo wa kwanza, wa pili kutoka kushoto) akiwakaribisha warusi
Serikali ya Urusi imesema maneno yake hayo "hayafai hata kidogo."
Ndege hizo mbili za kivita zenye uwezo wa kusafiri mwendo mrefu bila kutua zilitua katika uwanja wa ndege wa Simón BolÃvar viungani mwa mji mkuu wa Venezuela, Caracas, zikiandamana na ndege nyingine mbili za Urusi.
Waziri wa Ulinzi wa Venezuela Vladimir Padrino alisema ndege hizo ni sehemu ya mazoezi ya pamoja ya kijeshi kati ya Venezuela na mshirika wake Urusi.
"Hili tunalifanya kwa pamoja na marafiki zetu, kwa sababu tuna marafiki duniani ambao hutetea na kuheshimu uhusiano wa usawa."
Mzozo wa kiuchumi wa nchini Venezuela ni mbaya kiasi gani?
Zaidi ya watu milioni mbili wametoroka nchini Venezuela tangu mwaka 2014, hiyo ikiwa ni karibu 7% ya watu wote nchini hiyo.
Venezuela inasema kuwa Marekani imekuwa ikiendeleza vita vya kiuchumi ili kumaliza karibu miaka 20 ya utawala wa kisosholisti nchini humo.
Bwana Maduro analaumu sera za Marekani na vikwazo dhidi ya taifa lake kwa kusababisha viwango vya juu vya mfumko wa bei na uhaba wa bidhaa muhimu.
Mamia ya raia wa Venezuela wameondoka nchini Venezuela baada ya hali ya kiuchumi kuwa mbaya zaidi
Siku ya Jumatatu kampuni ya kutengeneza magurudumu ya magari ya Goodyear, ilitangaza kuwa itasitisha huduma zake nchini Venezuela.
"Lengo letu limekuwa la kuendelea na shughuli zetu hapa lakini hali ya kiuchumi na vukwazo vya Marekani zimefanya hali nchini kuwa ngumu," Goodyear ilisema katika taarifa yake.
Wafanyikazi wake nchini Venezuela wamepewa magurudumu kumi ya magari kama sehemu ya malipo yao.
Mshirika kadhaa ya ya kigeni ikiwa ni pamoja na Kellogg na Clorox, yamefunga shughuli zao Venezuela, kutokana na mzozo wa kiuchumi na vikwazo vya Marekani.
Maoni