MTEULE THE BEST
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kupiga kura hii leo juu ya azimio lililowasilishwa na Marekani linalolenga kuiwekea vikwazo zaidi Korea Kaskazini. Mapendekezo yanayohusiana na vikwazo hvyo vipya dhidi ya Korea Kaskazini yanaweza kuikosesha nchi hiyo kiasi ya dola bilioni moja katika mapato yake ya kila mwaka.Baada ya mwezi mmoja wa majadiliano, Marekani imefikia makubaliano na China ambayo ni mshirika mkubwa kibiashara wa Korea Kaskazini juu ya hatua zinazolenga kuzidisha mbinyo dhidi ya nchi hiyo ili iweze kusitisha shughuli zake za nyukilia pamoja na majaribio ya makombora. Mapendekezo hayo yanalenga kupiga marufuku mauzo ya nje ya rasilimali kutoka Korea Kaskazini yakiwemo madini kama vile makaa ya mawe na chuma pamoja na samaki.Iwapo azimio hilo litatetekelezwa na nchi zote basi hatua hiyo itaikosesha nchi hiyo karibu theruthi moja ya mapato yatokanayo na mauzo ya nje yanayokadiriwa kufikia dola bilioni tatu kwa mwaka hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mmoja wa wanadiplomasia aliyeshiriki majadiliano yanayohusiana na hatua hizo. Zikiungwa mkono na washirika wake kutoka barani ulaya, Japan, Korea Kusini pamoja na Marekani zimekuwa zikiweka msukumo kwa Umoja wa Mataifa zikitaka umoja huo uchukue hatua zaidi za vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini kufuatia hatua yake ya kufanya jaribio la kombora la kutoka bara moja kwenda jingine mnamo Julai 4 mwaka huu.
Maoni