MTEULE THE BEST
Tarehe 18, Desemba ni Siku ya Uhamiaji Duniani. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema suala la uhamiaji limekuwepo tangu jadi na utaendelea kuwepo siku zote.
Katibu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema jibu katika kushughulikia suala la uhamiaji ni ushirikiano mzuri wa kimataifa katika kuangazia sababu zinazochangia ongezeko la wahamiaji ili kuhakikisha manufaa yake yanasambazwa kwa usawa na haki za binadamu zinalindwa ipasavyo.
Umoja wa Mataifa umesema katika historia ya mwanadamu, uhamiaji umekuwa kielelezo cha kuonyesha ujasiri na ari ya watu binafsi kukabiliana na changamoto mbele yake ili kutimiza ndoto ya kuwa na maisha bora.
Katika ulimwengu wa sasa wa utandawazi pamoja na kuimarika katika teknolojia za mawasiliano na usafiri, kumechangia pakubwa katika kurahisisha kuhama kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa watu na kuongeza idadi ya watu ambao wana dhamira na uwezo wa kuhamia kwingine duniani.
Nyakati hizi za sasa zimetoa fursa na changamoto kwa jamii kote duniani na pia inatoa nafasi ya kuhusisha uhamiaji na maendeleo kwa jumuiya ya kimataifa kutizama kwa undani suala la je uhamiaji unaweza kuchangia vipi katika kuimarisha sekta ya kiuchumi na kijamii kwa wanakotokea wahamiaji na wafikapo.
UN: Uhamiaji pia una manufaa
Uhamiaji umefungamanishwa na manufaa katika siasa za kikanda, biashara, na utamaduni lakini licha ya hayo, uhasama dhidi ya wahamiaji unazidi kuongezeka duniani.
Wahamiaji kutoka Haiti wakijitayarisha kuingia mpaka wa Canada
Katika kuadhimisha siku hii ya uhamiaji, ulimwengu umetakiwa kushughulikia kwa uwazi changamoto, ugumu, matukio ya dharura na yasiyotarajiwa yanayoibuka kutokana na uhamiaji kwa kushirikiana zaidi kati ya nchi na kanda hadi kanda.
Umoja wa Mataifa unachangia pakubwa katika wajibu huu ikiwa na lengo la kuanzisha mijadala zaidi na ushirikiano zaidi miongoni mwa mataifa na kanda mbali mbali duniani ili uhamiaji liwe ni suala la kuchipuka kwa fursa na kukuza utangamano zaidi badala ya kuwa suala linalotizamwa kama mzigo na kitisho.
Mnamo tarehe 19 mwezi Septemba mwaka jana, Baraza kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la pamoja la nchi wanachama kujitolea kuwalinda wahamiaji na wakimbizi na kuimarisha maisha yao.
Makubaliano hayo yajulikanayo azimio la New York kuhusu wakimbizi na wahamiaji, linatilia msisitizo umuhumi wa nchi kuhakikisha haki za wakimbizi zinalindwa na wanapewa mazingira salama na maisha yao kuboreshwa kupitia hifadhi, elimu na huduma za afya.
Kauli mbiu ya mwaka huu ya maadhimisho ya siku ya uhamiaji duniani ni uhamiaji salama kwa ulimwengu unaosonga mbele. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema katika kuadhimisha siku hii wanatambua na kusherehekea mchango wa wahamiaji takriban milioni 258 duniani
Maoni