MTEULE THE BEST
Mbunge wa Marekani ameitisha uchunguzi kuangalia unyanyasaji wa watu 92 wenye uraia wa Somalia wakati walipokuwa wanafukuzwa nchini humo.
Keith Ellison, ni mwakilishi wa wilaya kwenye jimbo la Minnesota, ambalo lina idadi kubwa ya watu wa jamii ya Wasomali, aliyasema hayo wakati wa mkutano baina yake na waandishi wa habari ya kwamba, maafisa wa uhamiaji waliwafungia wahamiaji hao, na kuwanyima chakula , huduma ya kwanza na huduma za afya kwa ujumla.
Kituo cha habari cha Minnesota Radio (MPR) kimearifu kuwa ndege iliyowabeba watu hao waliowekwa kizuizini , iliondoka Marekani tarehe 7 Disemba mwaka huu lakini ikarudi Miami siku iliyofuata.
Inaarifiwa kwamba safari yao ilichukua saa 40 ikiwa ni pamoja na saa 23 ikiweka kituo katika mji mkuu wa Senegal.
Ripoti hiyo, ikinukuu kesi iliyotolewa na wanasheria wa wafungwa, inasema kuwa wahamiaji haramu 92 walisalia kizuizini , ilhali mikono yao ikiwa imeshikamana na viuno vyao, na miguu yao, iliunganishwa kwa saa 48.
Bw. Ellison alitoa wito kwa shirika la Uhamiaji na Utekelezaji wa Forodha (ICE) kujibu mfululizo wa maswali ndani ya saa 48, ikiwa ni pamoja na kwa nini ndege ilirudi Marekani.
Shirika la ICE , lilitaarifu kuwa ndege hiyo ilirejea Marekani, kutokana na 'wahudumu wa ndege kukosa muda wa mapumziko ya kutosha kutokana na hitilafu kwenye hoteli waliyokuwa wamefikia jijini Dakar,' .
Shirika hilo pia limekana shutuma za unyanyasaji na kusema kuwa hakukuwa na mtu aliyeumizwa hisia zake wakati wote wa safari hiyo.
Na kuongeza utetezi wao kwa kutanabahisha kuwa wafungwa hao 92, walifungwa kutokana na sababu za usalama dhidi ya abiria wengine waliokuwemo katika ndege hiyo.
Wafungwa wapatao 61, waliwahi kuhukumiwa kutokana na makosa kama vile uhalifu, ubakaji na mauaji.
Wanasheria wa wafungwa hao, wamepokea agizo la mahakama linalozuia wafungwa hao kutolewa nchini Marekani hadi tarehe 8 Januari mwaka ujao.
Hakimu wa mahakama hiyo ametoa agizo hilo kwa kusema kuwa watu hao walioko kizuizini katika jimbo la Florida waendelee kupewa huduma za kibinaadamu ikiwemo huduma za afya
Maoni