Wizara ya afya ya nchini Congo imesema idadi ya visa vya homa ya Ebola vilivyothibitishwa nchini humo vimeongezeka kutoka watu watatu na kufikia watu 14.
Wizara hiyo imesema mtu mmoja pekee ndiye aliyethibitishwa kufariki dunia ingawa kuna madai kwamba watu 25 wamefariki.
Maafisa wa afya wako mbioni kuidhibiti homa hiyo inayosambazwa na virusi na ambayo kwa sasa imethibitishwa katika mji wa Mbandaka wenye watu zaidi ya milioni moja. Mbandaka ni mji ambao hauko mbali na Mji Mkuu Kinshasa na uko katika Mto Congo ambao ni eneo lenye shughuli nyingi za usafiri.
Shirika la Afya Duniani, WHO limefanya kikao cha dharura leo na kutangaza kwamba tahadhari ya kuenea kwa maradhi hayo imeongezeka kutoka "juu" na sasa imefikia kuwa "juu mno". Shirika hilo linasema kuwa tahadhari katika nchi zilizoko katika kanda hiyo imeongezeka pia kutoka kiwango cha "wastani" na sasa imefikia kiwango cha "juu", ingawa tahadhari ya maradhi hayo kuenea dunia nzima inasalia kuwa ya "chini".
Visa 44 vya homa ya kuvuja damu vimerekodiwa
Kuzuka kwa Ebola kunasababisha kujaribiwa kwa chanjo mpya ya Ebola ambayo ilionekana kufanya kazi vyema Afrika Magharibi miaka michache iliyopita. Zaidi ya vipimo 4,000 vya chanjo hiyo vimewasili nchini Congo wiki hii huku vipimo zaidi vikitarajiwa kufika. Changamoto kuu itakuwa kuiweka chanjo hiyo katika hali ya baridi katika eneo ambalo lina miundo mbinu duni na umeme katika sehemu chache.
Chanjo ya Ebola ikiingia nchini Congo
Julien Raickman ni Mkuu wa Madaktari wasio na Mipaka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
"Tulijua jana kwamba kumethibitishwa kisa kimoja baada ya uchunguzi wa maabara katika mji wa Mbandaka. Kuanzia mwanzo wa kuzuka kwa maradhi haya," alisema Raickman. "Tumerekodi visa 44 vya homa ya kuvuja damu. Na ni homa ambayo tuliiona, visa vyote vitatu vya Ebola ambavyo vimethibitishwa," aliongeza Mkuu huyo wa MSF.
WHO itaita kikao cha wataalam wa kamati ya dharura baadae leo
Jambo ambalo linadhibitiwa lisitokee kwa sasa ni kuzuka kwa Ebola katika mji wa Kinshasa, mji wenye mamilioni ya watu ambao wengi wao wanaishi katika nyumba za mabanda zisizo na mfumo wa kutoa maji machafu.
Watu wengi Congo wanaishi katika mitaa ya mabanda isiyo na hali bora ya usafi
Baadae leo, WHO itaita kikao cha wataalam wa Kamati ya Dharura kutoa ushauri kuhusu njia za kimataifa za kulikabili janga hilo na iamue iwapo itabuni mpango wa dharura wa kushughulikia wasiwasi wa kimataifa kuhusiana na Ebola.
Tangu mwaka 1976, huu ni mlipuko wa tisa wa Ebola nchini Congo. Virusi vya ugonjwa huu vinasambazwa kwa watu kutoka kwa wanyama wa porini wakiwemo popo na tumbili. Hakuna tiba maalum ya Ebola. Dalili zake ni homa, kutapika, kuharisha, maumivu ya misuli na wakati mwengine kuvuja damu ndani na nje ya mwili. Ebola inaweza kusababisha vifo katika asilimia 90 ya visa
Maoni