Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Javad Zarif amesema nchi yake itahitaji uhakikisho kutoka mataifa mengine yenye nguvu duniani iwapo iendelee kutekeleza mkataba wa kinyuklia wa mwaka 2015, baada ya Marekani ikujitoa.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov alikutana na mwenzake huyo wa Iran mjini Moscow Jumatatu kujadili kile kinachoweza kufanyika kulinda makubaliano hayo na Iran baada ya uamuzi wa rais wa Marekani Donald Trump kujitoa katika mkataba huo.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Mohammad Javad Zarif
Iran jana iliupa Umoja wa Ulaya siku 60 kutoa uhakikisho wa kuendelea na utekelezaji wa makubaliano hayo ya kinyuklia baada ya uamuzi huo wa Marekani kujitoa. "Lengo lililokusudiwa la mazungumzo ni kupata uhakikisho kwamba maslahi ya watu wa Iran, yatalindwa," Zarif alisema katika mkutano na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov, kwa mujibu wa shirika la habari la Urusi TASS.
Lavrov alisisitiza kwamba Urusi na wadau wengine katika mkataba huo wa kinyuklia wanania ya kuuendeleza, ujumbe ambao umerejewa pia katika matamshi kutoka Umoja wa Ulaya yaliyotolewa na waziri wa masuala ya Ulaya wa Ujerumani Michael Roth.
"Shirikisho la Urusi pamoja na washiriki wengine katika mkataba huo wa kinyuklia, China, mataifa ya Ulaya, pia wana maslahi halali ambayo yamo katika makubaliano hayo yaliyoidhinishwa na baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, " alisema Lavrov.
"Leo tunamatumaini kuona ushiriki wa mataifa ya Ulaya, China, Urusi, Iran na Umoja wa Ulaya kwa kutumia utaratibu uliopo kutoruhusu kuporomoka kwa waraka huu muhimu, kutoruhusu kuivuruga hali katika eneo la mashariki ya kati, kutoruhusu vitisho vipya katika udhibiti wa kusambaa kwa silaha za kinyuklia."
Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza Boris Johnson akimpokea waziri mwenzake wa Iran Javad Zarif (Kulia)
Russia ambayo ina uhusiano imara na Iran, ilikuwa mpatanishi katika kupatikana kwa makubaliano hayo ya mwaka 2015 yenye lengo la kuizuwia Iran kujipatia silaha za kinyuklia.
Katika mkutano mjini Beijing mwishoni mwa juma, waziri wa mambo ya kigeni wa China Wang Yi alimuahidi Zarif kwamba China itaendelea kufanyakazi kuendelea na makubaliano hayo.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Mohammed Javad Zarif amesema mpango wa pamoja wa kuchukua hatua , uliotiwa saini mwaka 2015 ulikuwa katika msingi wa uwiano wa majukumu kati ya upande wa Iran na kulinda maslahi ya watu wa Iran ikiwa ni pamoja na Marekani."
Waziri anayehusika na masuala ya Ulaya wa Ujerumani Michael Roth
Mpango wa pamoja wa kuchukua hatua uko katika msingi wa uwiano wa majukumu kati ya upande wa Iran na Ulaya ikiwa ni pamoja na Marekani. Baada ya Marekani kujitoa uwiano huu uko hatarini. Tunapaswa kuona vipi tunaweza tunaweza kuulinda.
Mataifa matatu ya Ulaya, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza yameomba muda wa siku 90, duru mjini Tehran zimesema. Suala hilo linatarajiwa kuzungumzwa katika mkutano kati ya Zarif na wenzake wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels kesho Jumanne.
Maoni