Raisi wa Marekani Donald Trump amesema jeshi la maji la Marekani limetungua ndege isiyo na rubani ya Iran katika eneo la mpaka kati ya ghuba ya uajemi na ghuba ya Oman.
Amesema meli ya jeshi lake ''ilichukua hatua'' siku ya Alhamisi baada ya ndege hiyo kusogea kwa takriban mita 914 karibu na chombo hicho.
Iran haijasema chochote kuhusu hilo. Mwezi Juni, Iran iliangusha ndege ya kijeshi isiyo na rubani ya Marekani, na kusababisha hofu ya kutokea mzozo wa kijeshi.
Awali Tehran ilisema imekamata ''meli ya kigeni'' na wafanyakazi wake 12 siku ya Jumapili kwa kusafirisha mafuta kinyume cha sheria.
Iran imekuwa ikishutumiwa na Marekani kwa kushambulia meli zake tangu mwezi Mei.Tehran ilikana shutuma hizo.
Raisi Donald Trump amesemaje?
Akizungumza Ikulu, Trump amesema ''Ninataka kuwajulisha kuhusu tukio lililotokea kwenye eneo la mpaka wa Hormuz leo lililohusisha meli yetu ya kijeshi.
Chombo hicho kilichukua hatua ya kujilinda dhidi ya ndege isiyo na rubani ya Iran ambayo ilikuwa karibu sana hatua iliyokuwa ikitishia usalama wa meli na waliokuwa ndani ya meli hiyo. Ndege hiyo iliharibiwa mara moja''.
Hili ni tukio miongoni mwa matendo mengine ya uchokozi unaofanywa na Iran dhidi ya meli zinazokuwa kwenye maji ya kimataifa. Marekani in haki ya kujitetea, na kutetea maslahi yake''.
Washington awali ilisema Iran lazima haraka iachie meli ambayo ilidai kushikiliwa na Iran.
Vyombo vya habari vya Iran vilinukuu jeshi la Iran likisema kuwa meli hiyo ilikuwa imebeba lita 220,000 za mafuta.
Meli hiyo ilikamatwa kusini mwa Iran, kisiwa cha Larak, Iran ilieleza.
Chanzo ni nini?
Kumekuwa na mvutano katika eneo la Ghuba tangu Marekani ilipoweka vikwazo zaidi dhidi ya sekta ya mafuta ya Iran baada ya kujiondoa kwenye mkataba wa nyukilia wa Iran wa mwaka 2015.
Marekani imeishutumu Iran kwa mashambulizi mawili dhidi ya meli za mafuta katika eneo la ghuba ya Oman mwezi Mei na Juni, shutuma ambazo Iran imezikana.
Iran pia ilidungua ndege ya kijasusi ya Marekani katika eneo la mpaka huo. Tehran imesema ndege hiyo iliingia kwenye anga lake na tukio hilo lilituma ujumbe ''wa wazi kabisa kwa Marekani''.
Jeshi la Marekani limesema ndege isiyo na rubani ilikuwa ikiruka usawa wa eneo la maji ya kimataifa tukio ambalo limeelezwa kuwa ''shambulizi la kichokozi''.
Maoni