Barua mpya iliyovuja yadai Trump amevunja mkataba wa nyukilia 'ili kumkera Obama'
Rais Donald Trump ameachana na mkataba wa nyukilia wa Iran ili kumkera Barack Obama, hiyo ni kwa mujibu wa barua ya siri iliyovuja kutoka kwa aliyekuwa balozi wa Uingereza nchini Marekani.
Sir Kim Darroch alielezea hatua ya Trump kuvunja mkataba huo kama "ubadhirifu wa kidiplomasia" kwa mujibu wa gazeti la Mail on Sunday.
Gazeti hilo linadai kuwa barua hiyo iliandikwa baada ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Borris Johnson kuirai Marekani mwaka 2018 kusalia ndani ya makubaliano hayo.
Barua hii mpya inavuja katikakipindi ambacho polisis nchini Uingereza wameonya juu ya uchapishwaji wa barua hizo.
Barua ya kwanza kutoka kwa balozi huyo ambayo ilikuwa inakosoa utawala wa Trump ilivuja wiki moja iliyopita na kusababisha majibizano ya hasira baina ya Uingereza na Marekani.
Majibizano hayo yamesababisha Sir Kim kujiengua kwenye wadhifa wake licha ya serikali ya Uingereza kupitia Waziri Mkuu Theresa May kueleza kuwa inamuunga mkono.
Barua mpya iliyovuja inasema nini?
Gazeti la Mail on Sunday linaripoti kuwa Sir Kim alimwandikia Bw Johnson akimuelezea kuwa rais Trump kutoka chama cha Republican anavunja mkataba huo kwa sababu za "utashi binafsi" - kwa sababu makubaliano hayo yalifikiwa na mtangulizi wake kutoka chama cha Democrat, Barack Obama.
Kupitia mkataba huo, Iran ilikubali kuacha kurutubisha madini ya urani katika viwango vya kutilia mashaka na nchi za magharibi zikiongozwa na Marekani zikakubali kuiondolea nchi hiyo vikwazo vikali vya kiuchumi.
Trump alitangaza kuwa asingeshirikiana tena na Sir Kim Darroch (kulia) kabla ya balozi huyo kutangaza kujiuzulu Jumatano.
Hata hivyo, Trump alidai kuwa haamini kama makubaliano hayo yalisaidia kwa kina kuizuia Iran katika ndoto zake za kutengeneza silaha za nyuklia.Akaenda mbali zaidi kwa kurejesha vikwazo vya Marekani dhidi ya taifa hilo na kujitoa kwenye mkataba huo mwezi Mei 2018.
Balozi huyo wa Uingereza katika barua yake kwenda London inasemekana alieleza kuwa kulitokea mgawanyiko mkubwa miongoni mwa washauri wa rais Trump, na kuwa Ikulu ya White Haouse haikuwa na mpango thabiti wa kuliendea jambo hilo baada ya kujitoa kwenye makubaliano.
Katika barua hiyo, Sir Kim anadaiwa kuandika kuwa: "Matokeo yake ni kuwa kitendawili cha Ikulu ya White House kimeonekana: unaweza kumuona kila mtu kasoro rais mwenyewe: lakini katika uhalisia, utawala huu upo katika hali ya ubadhirifu wa kidiplomasia, kwa sababu za kiitikadi na utashi binafsi - maana yalikuwa ni makubaliano ya Obama.
"Na zaidi ni kuwa, hwana mpango thabiti wa baada ya kujitoa kwenye makubaliano; na vyanzo vyetu kutoka wizara ya mambo ya nje (ya Marekani) asubuhi hii vinaeleza kuwa hakuna mpango wowote wa kuwasiliana na washirika, iwe katika ukanda huu (Amerika) ama Ulaya."
Mzozo wa barua hizo umeendaje?
Sir Kim alijiuzulu ubalozi Jumatano akisema imekuwa ni vigumu kwake kuendelea na nafasi hiyo.
Barua ya kwanza kabisa iliyovuja ya Sir Kim, ilionesha kuwa balozi huyo akimuelezea Trump kama hakuwa mtu mwerevu na stadi.
Trump akajibu mapigo kwa kumita Sir Kim kuwa ni "mtu mpumbavu sana", na kuongeza kuwa asingeshirikiana naye tena.
Sir Kim alijivua wadhifa wake Jumatano akisema imekuwa ni vigumu kwake kuendelea na nafasi hiyo.
Johnson ambaye ndiye alikuwa akiandikiwa barua hizo kwa sasa ni mgombea wa nafasi ya Uwaziri Mkuu kupitia chama cha Conservative na ameshutumiwa vikali kwa kutoonesha kumuunga mkono hadharani Sir Kim kwenye mjadala wa runingawiki iliyopita.
Serikali ya Uingereza pia imeanzisha uchunguzi kujua imekuwaje barua hizo za siri zimevuja.
Maoni