Ruka hadi kwenye maudhui makuu

Chadema watoa taarifa kuhusu Jeshi la Polisi kumshikilia dereva wa Mbowe



Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimelalamikia hatua ya  Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kumshikilia kwa siku mbili  mtumishi wao Williard Urassa. 

Urassa ambaye ni dereva wa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alikamatwa jana nje ya chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. 

Taarifa iliyotolewa leo, Novemba 24, 2018 na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene imeeleza tangu Urassa alipokamatwa na polisi, jeshi hilo limekataa kumpatia dhamana huku likizuia mtu yeyote kuonana naye. 

Hii ndio Taarifa kamili: 

Kwa siku ya pili leo Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia Ndugu Williard Urassa, ambaye ni mtumishi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Makao Makuu, bila kueleza sababu za kumshikilia, huku pia akinyimwa haki zake za msingi, kinyume cha sheria za nchi. 

Ndugu Urassa ambaye ni Dereva wa Mwenyekiti wa Chadema Taifa, alikamatwa jana nje ya chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akiwa mmoja wa wananchi waliokuwa wakisikiliza kesi na. 112/2018 inayowakabili baadhi ya Viongozi Wakuu wa Chama na wabunge saba wa Chadema. 

Tangu alipokamatwa na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, jeshi hilo limekataa kumpatia dhamana huku pia likizuia mtu yeyote kuonana naye, wakiwemo wanasheria waliofika kwa ajili ya kumpatia msaada wa kisheria, hali ambayo inaibua maswali mengi na sintofahamu kubwa kuhusu hali yake baada ya kukamatwa. 

Tunalaani na kukemea vikali kitendo hicho cha Jeshi la Polisi ambacho ni mwendelezo wa tabia inayopaswa kuachwa mara moja ya jeshi hilo kujipatia mamlaka lisilokuwa nayo, hasa kuwakamata na kuwashikilia chini ya ulinzi kinyume cha sheria. 

Ni vyema jeshi hilo likatambua kuwa halina mamlaka ya kumshikilia mtu yeyote kwa namna hiyo, hivyo tunalitaka lieleze kwanini linamshikilia dereva huyo, apewe haki zake za msingi ikiwemo kuonana na ndugu na wanasheria na pia kuachiwa huru kwa dhamana. 

Imetolewa leo Jumamosi, Novemba 24, 2018 na; 

Tumaini Makene 
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano 
CHADEMA

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MAPENZI: Kuna faida na ni muhimu Mpenzi wako kuwa rafiki yako pia

Kuna faida kubwa kwa wapenzi kuwa marafiki KUTOKANA na mila mbalimbali, baadhi ya watu wamekuwa wakiamini kwamba mwanamke ni daraja la pili. Daraja la kwanza na lenye kuthaminiwa ni mwanaume. Yaani mwanamke hana kauli kwa mwanaume. Anakuwa kama mtumwa fulani hivi.  Mwanaume akiongea, basi ni maelekezo kama vile rais wa nchi anavyotoa maelekezo kwa watu walio chini yake. Hakuna wa kupinga. Akisema sitaki kitu fulani kifanyike, basi ni mpaka atakapotoa maelekezo mengine. Vinginevyo, maelekezo ya awali yatabaki kusimama kama sheria.  Wapo baadhi ya wanawake wanaofurahia aina hii ya uhusiano kwa sababu ya mazoea. Kwamba wamekuzwa hivyo, mwanaume ni mwanaume. Huu ni mfumo ambao watu wengi wamekuwa wakiuishi. Kuna ambao wanakubaliana nao, wengine hawakubaliani nao.  Watu wengi sana wamekuwa wakiishi katika malumbano katika mahusiano yao kutokana na mfumo huu wa maisha. Mwanamke hataki kuishi kama mtumwa, mume anakomaa kuonesha uanaume wake. Hakuna anayekubali kushuka,...

Urusi: Vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini havitafua dafu

MTEULE THE BEST Image caption Waziri wa maswala ya kigeni nchini Urusi Sergei Lavrov na mwenzeka wa Marekani Rex Tillerson Waziri wa maswala ya kigeni nchini Urusi Segei Lavrov amemwambia waziri wa ulinzi nchini Marekani Rex Tillerson kwamba kuiwekea vikwazo zaidi Korea Kaskazini hakutafua dafu. Taarifa iliochapishwa na wizara ya kigeni nchini Urusi inasema kuwa wawili hao walizungumza kwa njia ya simu na kushutumu majaribio ya makombora ya hivi karibuni yaliotekelezwa na Pyongyang . Lakini inasema kuwa bwana Lavrov alisisitiza kwamba diplomasia ndio njia ya pekee ya kumaliza wasiwasi katika rasi ya Korea, na kutaka hatua zozote dhidi ya taifa hilo kusitishwa akionya huenda zikasababisha madhara yasiojulikana. Waziri wa ulinzi nchini Marekani amesisitiza kuwa bado kuna fursa ya kidiplomasia katika kukabiliana na Korea Kaskazini. Mapema rais Trump alichapisha ujumbe katika akaunti yake ya Twitter akisema mazungumzo sio suluhisho.

Fuvu la binadamu wa kale liligunduliwa miaka 60 iliyopita nchini Tanzania

Fuvu la binadamu wa kale liligunduliwa miaka 60 iliyopita nchini Tanzania Miaka 60 siku kama ya leo ugunduzi mkubwa ulifanyika katika eneo la Olduvai Gorge, kwenye kreta ya Ngorongoro. Wanaakiolojia Louis na Mary Leakey waligundua fuvu la mtu anayeaminika kuwa ni wa kale zaidi waliyompa jina la Zinjanthropus. Ugunduzi huo uliofanyika saa nne asubuhi Julai 22, 1959 kipindi hicho kwenye eneo la Tanganyika ulikuwa wa vipande zaidi ya 100 ukasaidia katika kutambua asili ya watu wa awali duniani. Kabla ya ugunduzi huo, wanasayansi na wanahistoria walikuwa wakiamini kuwa binadamu wa kale walitokea Uchina baada ya ugunduzi wa mafuvu ya kale baina ya 1923 na 1927 nchini humo ya Homo eractus, ama maarufu kama Peking Man. Mafuvu hayo ya Uchina yalikuwa na umri wa takribani miaka 750,000. Mafuvu ya Olduvai eneo ambalo kwa sasa lipo Tanzania wakati wa ugunduzi wake lilikuwa na umri wa takribani miaka milioni 1.75, na hakuna mabaki ya mtu wa kale zaidi ambayo mpaka sasa yamegundul...