Mwanamfalme Mohammed Bin Salman wa Saudi Arabia na Rais Trump wa Marekani
Rais wa marekani Donald Trump ametetea uhusiano wa karibu uliopo kati ya marakeni na Saud Arabia bila kujali lawama juu ya mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoogi yanayoiandama Saud Arabia.
Trump amesisitiza kuwa huenda mwanamfalme Mohamed Bin Salman alijua kuhusu mauaji lakini uhusiano uliopo ni baina yake na Saud Arabia na hawezi kuupoteza.
Rais huyo wa nchi yenye nguvu zaidi duniani amewaambia waandishi wa habari kuwa asingependa kuharibu uchumi wa dunia kwa kuwa na mahausiano mabaya na Saud Arabia.
''Siwezi kuwambia nchi inayotumia pesa zake nyingi na imenisaidia kitu kimoja kikubwa sana, bei ya mafuta, sasa imetulia haipandi wala kushuka, hivyo siwezi kuharibu uchumi wa dunia kwa kuanza kuwa na uhusiano mbaya na Saud Arabia, siwezi kuharibu uchumi wa dunia na uchumi wa nchi yetu''.
Trump ameongeza pia, kuvunja uhusiano na Saud Arabia ni sawa na kuachia pesa nyingi ziende kwa mataifa mengine kama Urusi na China.
Khashoggi alikuwa mkosoaji kinara wa sera za Saudia hasa zile za mwanamfalme bin Salman
''Ni marekani kwanza kwangu mimi, hatuwezi kuachia mabilioni ya pesa yaende kwa Urusi na China, na watu wengine wazipate, ni kuhusu mimi , ni rahisi tuu, marekani kwanza, na tukivunja huu uhuasiano mtaona bei za mafuta zitakavyopanda, sasa hivi nimeziweka chini, na wamenisaidia kufanya hivyo , na ningependa bei ishuke zaidi.''
Kuhusu mwanamfalme bin Salman kuhusika na mauaji , trump amesema inawezekana Bin Salman alikua akijua kuhusu tukio hilo ama asiwe ana taarifa yoyote.
Uchunguzi wa shirika la kijasusi la nchi hiyo CIA ulioripotiwa na vyombo vya habari vya Marekani unaonesha kuwa uwezekano ni mkubwa kuwa bin Salman aliidhinisha mauaji ya Khashoggi. Lakini Trump anasema uchunguzi huo haujakamilika kwa asilimia 100.
Khashoggi aliuawa ndani ya ofisi za ubalozi wa Saudia mjini Istanbul Uturuki alipoenda kuchukua nyaraka kuhusu talaka yake na aliyekuwa mkewe nchini Saudia. Khashoggi alikuwa mkosoaji kinara wa sera za Saudia hasa zile za bin Salman na alikimbilia uhamishoni Marekani mwaka 2017 akihofia usalama wake.
imesema kuna uwezekano mkubwa kuwa mwanamfalme bin Salman alijua kuhusu mipango ya mauaji ya Khashoggi
Kwa upande wa Saud Arabia wamekuwa wakikanusha uhusika wa Bin Salman katika tukio hilo. Awali walikanusha kabisa kutokea kwa mauaji hayo lakini baada ya kubanwa walikiri na kulaumu oeresheni haramu iliyofanywa na maaisa usalama wa nchi hiyo.
Mwanamfalme wa Saudia aliamini 'Khashoggi alikuwa hatari'
Kauli ya Trump inawapa nafuu viongozi wa Saudia ambao wamekuwa wakipitia wakati mgumu kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa kutokana na mauaji hayo. Bado mwili wa mwanahabari huyo haujapatikana na inaaminika ulitoswa kwenye tindikali ili kupoteza ushahidi.
Hata hivyo, wakosoaji wa Trump wameshtushwa na kauli yake ya kuitetea Saudia. Tayari wajumbe wa Bunge la Wawakilishi la Marekani kutoka vyama vyote viwili vya Republican na Democrat wametishia kuwasilisha muswada wa kuiwekea vikwazo nch ya Saudia.
Katika maelezo yake, Trump aliisifia Saudia kuwa mshirika imara katika kuibana Iran katika programu yake ya matumizi ya teknolojia ya nyuklia.
Maelezo hayo ya Marekani yamepingwa vikali na Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran Javad Zarifambaye amesema ni ajabu kuona Trump anatumia jina la Iran katika utetezi wa tukio hilo, "Itakuwa Iran pia imesababisha moto wa nyika unaoendelea California. Maana sasa kwenye kila shida inayoikumba Marekani, Iran tunahusishwa
.
Maoni