Dkt. Mwakyembe : Woga wa kukopa ni tatizo kubwa kwa Watanzania
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amesema Watanzania waache kuogopa kukopa lakini benki nazo zibadilike.
Dkt. Mwakyembe amesema, woga wa kukopa ni tatizo kubwa kwa Watanzania na ni la kihistoria kwa kuwa zamani kuliko na sheria iliyowazuia wazawa wasikope kwa sababu iliwatambua kuwa ni watoto.
Waziri Mwakyembe amewaeleza wajumbe wa Jukwaa la Fursa za Biashara Mkoa wa Tabora hali sasa imebadilika hivyo wananchi wakope wawekeze.
Tabora inabidi ibadilike hasa, isiwe Tabora ile ya maembe tunagawana na wadudu” amesema na pia amewaeleza viongozi kuwa uongozi si umasikini.
Dkt. Mwakyembe amesema, viongozi hawazuiwi kuwa matajiri ila watapaswa kueleza wameupata vipi utajiri huo na ndiyo maana kuna suala la maadili kwa viongozi wa umma.
Mwakyembe alikuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Fursa za Biashara Tabora lililofanyika kwa siku tatu mjini Tabora. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alilifungua jukwaa hilo juzi.
Viongozi mbalimbali wamehudhuria jukwaa la Tabora akiwemo Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Joseph Kakunda, wabunge kutoka mkoani humo, Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Magazeti ya Serikali, Hab Mkwizu, na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora, Hassan Wakasuvi.
Viongozi wengine waliohudhuria jukwaa hilo ni wakuu wa wilaya, watendaji wakuu wa mkoa huo, wakurugenzi watendaji wa Halmashauri, makatibu tawala wa wilaya, wenyeviti wa halmashauri za wilaya, wakuu wa taasisi na waendai wengine mkoani humo
Maoni