Mtanzania Joyce Msuya ateuliwa kaimu kiongozi wa shirika la UNEP lenye makao yake Nairobi
UN
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amemteua Mtanzania Joyce Msuya kuwa kuwa kaimu kiongozi wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira, UNEP.
Bi Msuya amekuwa Naibu Katibu Mkuu na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo ambalo lina makao makuu yake jijini Nairobi, Kenya.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amenukuliwa na vyombo vya habari vya kimataifa akisema Antonio Guterres amechukua hatua hiyo huku akiendelea kumtafuta mkuu wa kudumu wa UNEP.
Wadhifa wa kiongozi wa UNEP ulikuwa umebaki wazi baada ya kujiuzulu kwa Erik Solheim ambaye amekumbwa na kashfa kuhusu gharama yake ya matumizi katika safari.
Mswada wa ripoti ya ukaguzi wa fedha ambayo ilipatikana na gazeti la Uingereza la Guardian, na ambayo BBC imefanikiwa kuisoma, inaonyesha Solheim alitumia jumla ya $488,518 (£382,111) akisafiri siku 529 kati ya siku 668.
Alikuwa hayupo afisini kwa takriban asilimia 80 ya muda wake kazini.
Ripoti hiyo inasema gharama hiyo imetia doa sifa za UN kama shirika ambalo huangazia masuala ya uhifadhi wa mazingira na uendelevu.
Erik Solheim alikuwa mkurugenzi mtendaji wa UNEP
Hakukuwa na mtu yeyote wa kufuatilia au kuwajibika kuhusu safari za kiongozi huyo.
Solheim amesema anatumai hatua yake ya kujiuzulu italifaa shirika hilo, na Umoja wa Mataifa kwa jumla.
Tajriba ya Bi Msuya
Bi Msuya aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo mwezi Mei mwaka huu kuchukua nafasi ya Ibrahim Thiaw wa Mauritania, ambaye alikuwa amemaliza muda wake wa kuhudumu.
Hadi wakati wa kuteuliwa kwake, Bi Msuya alikuwa mshauri wa Makamu Rais wa Benki ya Dunia kwa ukanda wa Asia Mashariki na Pacific jijini Washington, DC wadhifa alioushikilia tangu mwaka jana.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, kwa mujibu wa UN alisema, wakati wa kuteuliwa kwake kwamba, "Bi Msuya analeta uzoefu wake wa zaidi ya miaka 20 kwenye nyanja za maendeleo ya kimataifa kuanzia masuala ya mashirika, mikakati, uendeshaji, ufahamu wa usimamizi na ubia alioupata wakati akifanya kazi huko Afrika, Amerika Kusini na Asia."
Daktari Mtanzania atambuliwa Marekani
Mtanzania afungua mgahawa Sweden
Mtanzania aliyemaliza wa mwisho Olimpiki ya 1968
Moshi: Mtanzania aliyeamua kutokufa moyo Olimpiki
Alishika nyadhifa mbalimbali katika ngazi ya uandamizi kwenye Benki ya Dunia ikiwemo mwakilishi wa Benki ya Dunia na Mkuu wa ofisi ya benki hiyo hiyo Korea Kusini na mratibu wa taasisi ya Benki ya Dunia inayosimamia Asia Mashariki na Pasifiki nchini China.
Joyce Msuya
✔@JoyceMsuya
Nimekutana na timu ya Tanzania ya umoja wa mataifa. Timu ina mfano mzuri wa mfumo wa kufanya kazi kwa pamoja "Delivering as one" @UNEnvironment inalenga kuendelea kuwezesha kukabiliana na changamoto za mazingira na mabadiliko ya tabia nchi Tanzania @UmojaWaMataifa @undptz
129
20 people are talking about this
Mwisho wa ujumbe wa Twitter wa @JoyceMsuya
Naibu Mkurugenzi Mtendaji huyo mteule wa UNEP ana shahada ya uzamivu kwenye masuala ya sayansi ya biolojia ya viumbe viini na viumbe vidogo pamoja na sayansi ya kinga mwilini kutoka Chuo Kikuu cha Ottawa, Canada.
Ana shahada ya kwanza katika biokemia na kinya mwilini kutoka Chuo Kikuu cha Strathclyde, Scotland.
Bi Msuya ameolewa na ana watoto watatu.
Maoni