Msanii wa filamu nchini, Wema Sepetu leo amefika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kusikiliza kesi inayomkabili ambapo anashtakiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa tuhuma za kuchapisha na kusambaza video za maudhui ya ngono mitandaoni.
Msanii Wema Sepetu, akiwa na mama yake mzazi Mariam Sepetu.
Wema amefika mahakamani hapo majira ya saa 3 asubuhi akiongozana na mama yake mzazi, Mariam Sepetu na wakili wa msanii huyo, Reuben Simwanza, na kwenda moja kwa moja hadi kwenye ukumbi wa mahakama hiyo kusubiri kuanza kusikilizwa kwa kesi yake.
Shauri la kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa katika Maakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya hakimu, Maira Kasonde huku Wakili wa utetezi akiwa Ruben Simwanza na upande wa Jamhuri ukisimamiwa na Wakili Jenifer Masue, lakini imeahirishwa hadi Desemba 12 mwaka huu kutokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika.
Novemba 1, 2018 Wema alipandishwa katika mahakama hiyo akikabiliwa na shtaka la kusambaza video ya ngono kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram, kesi yenye jalada namba KJN/ RB/13607/2018-KUCHAPISHA NA KUSAMBAZA MAUDHUI YA NGONO MTANDAONI.
Wema alisomewa shtaka hilo mbele ya Hakimu Mahira Kasonde ambapo alikana kosa hilo kisha kuachiwa kwa dhamana ya Shilingi milioni 10 kupitia kwa Salim Limu, ambapo Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 20, mwaka huu (jana) ambapo haikusikilizwa kwa sababu ilikuwa ni Sikukuu ya Maulid.
Kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, endapo mtuhumiwa atabainika kusambaza picha au video za ngono au zinazoashiria vitendo vya ngono, adhabu ya kosa hilo ni pamoja na faini ya shilingi milioni 20 au kifungo kisichopungua miaka saba jela au vyote kwa pamoja
Maoni