Rais Mnangagwa alikaribishwa rasmi na mwenyeji wake rais John Magufuli
Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa yuko Dar es salaam katika ziara ya kwanza nchini humo tangu aingie madarakani.
Ni ziara ya siku mbili ambayo imetajwa kulenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, mwenyeji rais wa Tanzania John Pombe Magufuli na Rais Mnangagwa wamekubaliana kuimarisha biashara na uwekezaji baina ya mataifa hayo mawili yaliotajwa kuwa na udugu wa kihistoria.
Mnangagwa amewasili asubuhi hii na kupokewa na rais Magufuli katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Akiwa Tanzania kiongozi huyo anatarajiwa kutembelea chuo cha kilimo alikosomea miongoni mwa wapiganjiaji uhuru waliotoka nchi za kusini mwa Afrika.
Kukuza uhusiano wa Zimbabwe na Tanzania:
Tanzania ilikuwa na jukumu muhimu katika mataifa ya Afrika yaliojikomboa dhidi ya utawala wa wazungu.
Makao makuu ya muungano wa Afrika wakati huo ukijulikana kama (OAU), yalikuwa mjini Dar es Salaam ambapo mikakati iliidhinishwa kumegua utawala wa kikoloni katika nchi za Afrika.
Katika taarifa kutoka ikulu Tanzania, Rais Magufuli amesema wamekubaliana tume ya pamoja ya ushirikiano, iliyokutana mwisho mnamo 1998, ikutane mara baada ya uchaguzi mkuu wa Zimbabwe mwezi ujao ili kujadili vikwazo na kutafuta majawabu ya kukuza biashara na uwekezaji baina ya Mataifa haya mawili.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Tanzania, Said Msonga anaamini huenda Rais Mnangagwa anatumia ziara hii kama mbinu ya kutaka kuibua hisia za wanamchi na kutaka kuonekana mzalendo na kumtengenezea mazingira ya kushinda uchaguzi.
Kadhalika anaeleza huenda hii ni fursa kwake kuweza kuyahifadhi mahusiano kati ya mataifa hayo mawili baada ya uchaguzi.
Rais Magufuli na Rais Mnangagwa wamekubaliana kuimarisha biashara na uwekezaji baina ya mataifa hayo mawili
Na kuwa na manufaaa ya kiuchumi na kidiplomasia kwa nchi zote mbili.
Itakumbukwa kwamba Rais Magufuli alikuwa miongoni mwa viongozi wa Afrika waliompongeza rais Mnangagwa kwa kuchukua uongozi wa nchi pasi kushuhudia ghasia za aina yoyote.
Ziara hii inafuata mualiko rasmi kwa Mnangagwa kutoka rais Magufuli uliowasilishwa na ujumbe wa chama tawala CCM ulioongozwa na aliyekuwa katibu mkuu Abdulrahman Kinana waliokwenda Zimbabwe mwezi uliopita.
Kinana alifanya ziara hii mwishoni mwa mwezi may kabla ya kuachia ngazi kama katibu mkuu wa CCM.
Mnangagwa, aliingia madarakani mnamo Novemba kufuatia mapinduzi ya jeshi dhidi ya kiongozi mkongwe Robert Mugabe.
Uchaguzi mkuu nchini Zimbabwe wa kwanza baada ya utawala wa Mugabe unatarajiwa Julai 30
Maoni