MTEULE THE BEST
Zitto Kabwe amefunguka na kusema kitendo cha Makamu wa Rais Mhe. Samia kupokelewa na Balozi Kenya ni ishara kuwa mahusiano ya Tanzania na Kenya hayapo vizuri na kudai Rais Magufuli kutokwenda kwenye sherehe za kuapishwa Kenyatta inaweza kueleweka.
Zitto Kabwe amesema hayo kupitia mtandao wake wa twitter na kusema kitendo cha Rais Magufuli kutohudhuria kwenye sherehe za kuapishwa kwa Rais mteule wa Kenya Uhuru Kenyatta inaweza kueleweka kwani kiongozi huyo hakuweza kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame.
"Makamu wetu wa Rais kupokelewa na Balozi ( sio hata Waziri wa Mashauri ya Kigeni au Waziri mwengine) ni dalili kuwa mahusiano yetu yanalega lega. Rais kutokwenda Kenya inaweza kueleweka maana hata Rwanda hakwenda kwenye uapishaji wa Paul Kagame" aliandika Zitto
TAARIFA ZAIDI
MAGUFULI
Rais John Pombe Magufuli
Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amemtuma makamu wake wa rais kumwakilisha katika sherehe ya kuapishwa kwa rais Uhuru Kenyatta nchini Kenya.
Rais Magufuli ambaye awali alikuwa amethibitisha kuhudhuria sherehe hiyo na hata kutuma taarifa kwa vyombo vya habari sasa amemtuma makamu wake Mama Samia Suluhu Hassan kumwakilisha.
Uhusiano kati ya Kenya na Tanzania umeonekana kudorora siku za karibuni hasa kufuatia kupigwa mnada kwa ng'ombe zaidi ya elfu moja kutoka Kenya waliokuwa wameingizwa Tanzania. Tanzania kadhalika ilichoma moto vifaranga waliodaiwa kutoka Kenya.
Tayari kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Edward Lowassa ambaye ni rafiki mkubwa wa rais Uhuru Kenyatta amewasili katika uwanja wa Kasarani tayari kwa sherehe hiyo.
Rais Magufuli ni mwandani wa karibu wa kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ambaye alisusia uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26 ambao Uhuru Kenyatta aliibuka mshindi kwa kujipatia asilimia 98 ya kura zilizopigwa.
Tayari makamu huyo anatarajiwa kuwasili katika uwanja wa Kasarani wakati wowote sasa
Maoni