Italia imetumbukia katika mgogoro mpya wa kisiasa baada ya kusambaratika kwa jaribio la vyama vinavyofuata siasa za kizalendo kuchukua madaraka. Hii ni baada ya Waziri Mkuu mtarajiwa Giuseppe Conte kujiuzulu
Rais wa nchi hiyo Sergio Mattarella anatarajiwa kumteua mchumi anayeunga mkono sera za kubana matumizi kuiongoza serikali ya watalaamu kabla ya uchaguzi mpya. Rais Sergio Mattarella alitumia kura ya turufu kupinga uteuzi wa kiongozi anayekosoa vikali sera za Ulaya Paolo Savona kuwa waziri wa uchumi, hatua iliyovikasirisha vyama vya upinzani vya Five Star Movement na the League cha siasa kali za mrengo wa kulia na kusababisha waziri mkuu wao mteule Giuseppe Conte kujiuzulu.
Conte, mwenye umri wa miaka 53, ambaye ni wakili asiye na ujuzi wa kisiasa alitangaza kuwa ameachana na juhudi zake za kuunda serikali ya mabadiliko, hatua iliyoitumbukiza nchi hiyo katika mgogoro wa kisiasa karibu miezi mitatu baada ya uchaguzi mkuu wa Machi ambao haukutoa mshindi wa wazi. "Kama ilivyotarajiwa, nimerejesha mamlaka yangu niliyopewa na rais wa Jamhuri, Mattarella, ya kuunda serikali ya kuleta mabadiliko. Nimefanya juhudi kubwa, na kujitolea katika jukumu hili na hili limefikiwa katika mazingira yenye ushirikiano kamili na viongozi wa kisiasa walionipendekeza".
Rais Marttarella amekubali kujiuzulu kwa Conte
Rais Mattarella alikubali kila waziri aliyependekezwa isipokuwa Savona, ambaye aliitaja kanda ya euro kuwa sawa na "kizimba cha Ujerumani” na kusema kuwa Italia inahitaji mpango wa kujiondoa katika kanda hiyo ya sarafu ya euro kama itabidi kufanya hivyo. "Profesa Conte, ambaye namthamini na kumshukuru, ameniletea orodha ya majina ya mawaziri, ambayo nastahili kikatiba kuchukua jukumu la kuisaini orodha hiyo. Kwa hiyo rais wa jamhuri ana jukumu la dhamana, ambalo haliwezi kuchukuliwa na nafasi nyingine ya kisiasa. Nimeidhinisha mapendekezo yote ya mawaziri, lakini sikuidhinisha jina la waziri wa uchumi"
Viongozi wa vyama vya Five Star na the League, Luigi Di Maio na Matteo Salvini, walilaani kura hiyo ya turufu, wakilalamikia kile walichokiita kuwa ni uingiliaji unaofanywa na Ujerumani, mashirika ya viwango vya ukopeshekaji na mashirika ya kifedha.
MADA ZINAZOHUSIANA
Rais Mattarella amemuita Carlo Cottarelli, mchumi ambaye awali alifanya kazi na Shirika la Fedha la Kimataifa – IMF, kwa ajili ya mazungumzo leo, huku kukiwa na uvumi kwamba Cottarelli ataombwa kuunda serikali ya mpito wakati Italia ikikabiliwa na uwezekano mkubwa wa kuitisha uchaguzi wa mapema.
Cottarelli, mwenye umri wa miaka 64, alikuwa mkurugenzi mkuu wa idara ya masuala ya kifedha ya IMF kuanzia 2008 hadi 2013 na akajulikana kama "Bwana Mkasi” kwa kukata au kupunguza gharama ya matumizi ya fedha za umma nchini Italia.
Atakabiliwa na upinzani mkali wa kupewa ridhaa ya bunge huku kwa sababu vyama vya Five Star na the League vina wingi wa viti katika mabunge yote mawili
Maoni