Mmiliki wa klabu ya Chelsea Roman Abramovich, amesitisha upanuzi wa uwanja wa Stamford bridge unaomilikiwa na klabu hiyo kutokana na nchi hiyo kushindwa kushughulikia kibali chake cha kuishi nchini humo.
Abramovich tayari alikuwa ameshaweka mezani kiasi cha Paundi bilioni 1, kwaajili ya utekelezaji wa mpango huo, lakini amesimamisha ujenzi usianze hadi atakapojua hatima ya kibali chake cha kuishi.
BBC wameripoti kuwa Visa ya Roman Abramovich ambaye ni raia wa Urusi, imekwisha muda wake ndani ya wiki kadhaa sasa, lakini amekuwa akicheleweshwa kupatiwa kibali kutokana na mvutano wa kidipromasia kati ya Uingereza na Urusi.
Roman mwenyewe amesisitiza kuwa hawezi kuwekeza kwenye nchi ambayo hana kibali cha kuishi huku akieleza kuwa kitendo hicho hakiingiliani na shughuli zingine za uendeshaji wa klabu hiyo.
Tukio la kupewa sumu kwa jasusi wa zamani wa Urusi aliyekuwa nchini Uingereza Sergei Skripal, mapema mwaka huu, ndio limeelezwa kuwa chanzo cha ushirikiano mdogo kati ya nchi hizo mbili. Uwanja wa Stamford Bridge unachukua mashabiki 41,631 na ukipanua utaweza kuingiza 60,000.
Maoni