Katibu mkuu mpya wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally, ameeleza dhamira yake ya kusimamia misingi ya waasisi wa chama hicho ikiwemo azimio la Arusha pamoja na Katiba ya Chama hicho kikongwe nchini Tanzania.
Akizungumza kwa njia ya simu kwenye kipindi cha East Africa BreakFast kinachorushwa na East Africa Radio, Dkt. Bashiru amefunguka dhamira yake ya kukiimarisha chama kwa kutetea wanyonge na kujenga imani kwa wanachama na watanzania wote.
“Nafasi hii nimepewa ikiwa imeshakaliwa na watu wakubwa, nampongeza sana rafiki yangu Abdulrahman Kinana, kwa kukiacha chama kikiwa madarakani. Natarajia kwamba ataendelea kutoa mchango wake wa ushauri, akiwa na wenzake wengine waliostaafu katika utumishi wa chama, upande wa hadhi yangu mimi sina jipya, tunalo azimio la Arusha, tunayo itikadi ya ujamaa na kujitegemea, tunayo katiba ya chama, tunayo katiba ya nchi, hiyo ndiyo miongozo yetu kwahiyo mie sina jipya, mbali nakuwaahidi utumishi, utumishi ulio katika misingi ya miongozo ya vitu hivyo nilivyovitaja..” , amesema Dkt. Bashiru.
Baada ya uteuzi huo wa Dkt. Bashiru kama Katibu Mkuu mpya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kiongozi huyo anaweka historia ya kuwa katibu mkuu wa nane akipokea kijiti hicho toka kwa Ndugu Abdulrahman O. Kinana ambaye amejiuzulu nafasi yake hiyo.
Hii Hapa orodha ya makatibu wakuu wa CCM Tangu Mwanzo.
Pius Msekwa
Rashid M. Kawawa
Dk. Lawrence M. Gama
Mh. Philip Mangula
Yusuph makamba
Wilson Mukama
Abdulrahman O. Kinana
Dk. Bashiru A. Kakurwa
Maoni