Klabu za soka za Simba na Yanga zinaweza kukutana kwa mara ya nne msimu huu, endapo zitafuzu hatua ya nusu fainali ya michuano ya (SportPesa Super Cup) ambayo inafanyika katika msimu wake wa pili safari hii ikiwa nchini Kenya.
Vigogo hao wa soka ya Tanzania watatakiwa kushinda mechi zao za kwanza za michuano hiyo wakianzia Robo Fainali ambapo Simba SC atacheza na Kariobangi Sharks Juni 3 na Yanga wakikipiga na Kakamega Homeboys Juni 4.
Kwa msimu huu, tayari Simba na Yanga zimekutana mara tatu, wakianza Agosti 23 kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii mwaka 2017, mechi ambayo humkutanisha bingwa wa VPL na bingwa wa Kombe la FA. Katika mchezo huo Simba ilishinda kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0.
Timu hizo tena zilikutana katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Oktoba 28, 2017 na kutoka sare ya 1-1, Simba wakitangulia kwa bao la Shiza Kichuya dakika ya 57, kabla ya Obrey Chirwa kuisawazishia Yanga dakika ya 60.
Mechi ya tatu ilipigwa Aprili 29, mwaka huu ambapo bao la mlinzi, Erasto Edward Nyoni dakika ya 37 likaipa Simba SC ushindi wa 1-0, mechi zote hizo zikichezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
Maoni