Nchi washirika wa Marekani zimekasirishwa na hatua za serikali ya Rais Donald Trump kuziwekea vikwazo vya kiushuru, vinavyolenga bidhaa za chuma cha pua na bati. Umoja wa Ulaya, Canada na Mexico, zimeapa kulipiza kisasi.
Canada na Mexico zilitangaza mara moja hapo jana hatua za kujibu ushuru mpya uliowekwa na Marekani dhidi ya bidhaa zao za chuma cha pua na bati zinazoingizwa kwenye soko la nchi hiyo, nao Umoja wa Ulaya umesema tayari umejipanga kuujibu uamuzi huo wa serikali ya Trump. Waziri wa fedha wa Ujerumani Peter Altmeier amezungumzia uwezekani wa kushirikiana na Canada pamoja na Mexico, kuratibu mkakati wa pamoja dhidi ya Marekani.
Tangazo hapo jana kutoka kwa waziri wa biashara wa Marekani Wilbur Ross la kuanzisha rasmi vikwazo vya kiushuru dhidi ya Umoja wa Ulaya, Canada na Mexico lilihitimisha kipindi cha miezi kadhaa ya sintofahamu, juu ya iwapo Marekani ingeelea kuziondoa nchi hizo kwenye orodha yake ya vikwazo vya kibiashara.
Ulaya yakasirishwa
Katika hatua hizo, bidhaa zote za chuma cha pua zinazoingizwa Marekani kutoka Umoja wa Ulaya, Canada na Mexico ushuru wake umeongezwa kawa asilimia 25, na ongezeko la asilimia 10 limewekwa dhidi ya bidhaa za bati. Akizungumza mjini Brussels muda mfupi baada ya uamuzi wa Marekani, Rais wa kamisheni ya Ulaya Jean Claude Juncker alionekana dhahiri kuchukizwa, aliulaani uamuzi huo.
Rais wa Kamisheni ya Ulaya Jean Claude Juncker amesema Ulaya haitajikunyata mbele ya vikwazo vya Marekani
''Hii ni siku mbaya kwa biashara ya dunia. Ulaya haiwezi kukaa kimya kuhusiana na hatua kama hizi. Tutafikisha mara moja malalamiko katika Shirika la Kimataifa la Biashara, na mnamo saa chache zijazo, tutaweka wazi mpango wetu wa kulipiza kisasi.'' Amesema Juncker na kuongeza kuwa inachoweza kukifanya Marekani dhidi ya Ulaya, Ulaya pia inaweza kukifanya dhidi ya Mareakni.
''Haikubaliki hata kidogo kwamba nchi moja inaweza kujichukulia hatua kivyake katika biashara ya kimataifa.'' Amelalamika Juncker.
Macron amponda Trump
Ikulu ya Ufaransa mjini Paris imesema Rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron alizungumza na Rais Trump baada ya vikwazo hivyo kutangazwa, na kumweleza wazi kwamba kwa hatua hizo, Marekani imefanya makosa, na imevunja sheria. Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau pia amemkosoa vikali rais Trump, na tayari Canada imetangaza ushuru mpya kwa bidhaa za Marekani zenye thamani ya dola bilioni 12.8. Mexico pia imebainisha kuwa itaziongezea ushuru bidhaa za kilimo kutoka Marekani katika mzozo huo.
Rais Donald Trump amewapuuza wanaokosoa sera zake za biashara
Upinzani dhidi ya vikwazo hivyo vya ushuru vilivyowekwa na utawala wa Trump haukuja tu kutoka nchi zilizolengwa, bali pia kutoka Marekani kwenyewe. Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani Paul Ryan ambaye ndiye afisa wa ngazi ya juu zaidi wa chama cha Republican anachotoka Trump, amesema hakubaliani na rais huyo.
Ryan amesema badala ya kuzilenga nchi washirika, utawala wa Trump ungekuwa unashirikiana nao kuibana China, ambayo amesema kwa maoni yake, ndio yenye matatizo. Trump amezipuuza kauli zote zinazomkosoa, akisema enzi za Marekani kudhulumiwa kibiashara zimefika kikomo.
Wataalamu wa masuala ya uchumi wanasema Marekani haiwezi kuepuka kuumizwa na hatua zake yenyewe. Baadhi ya athari zinazotabiriwa ni kupanda kwa bei za bidhaa zitokanazo na chuma cha pua na bati, na kupotea kwa maelfu ya ajira
Maoni