Enzi mpya imeanza katika chama tawala nchini Tanzania CCM baada ya msomi wa chuo kikuu cha Dar es Salaam, Dk Bashiru Ally kukabidhiwa ofisi na mtangulizi wake Abdulrahman Kinana siku ya Alhamis(31.05.2018).
Msomi huyo aliyesifika kutokana na uchambuzi wa masuala ya siasa na kupenda kushiriki mijadala ya majukwaani sasa ameingia kwenye ulingo halisi wa kisiasa na anatazamiwa kuanza kukabiliana na hoja kutoka upinzani ambao wakati fulani alikaa nao meza moja kupigania yale yanayoonekana kuwa ni masuala ya pamoja ya kitaifa.
Ujio wake ndani ya CCM tayari umezusha mjadala wa hoja hasa kutokana na misimamo yake aliyokuwa akiionyesha wakati alipokuwa akishiriki kwenye mijadala ya wazi ikiwamo ile iliyohusu hali ya kisiasa nchini na umuhimu wa kuwa na katiba mpya.
Katibu mkuu mpya wa CCM Dr. Bashiru Ally aliyekuwa mhadhiri UDSM
Katika moja ya mijadala hiyo, msomi huyo ambaye anatajwa kuwa ni mtu mwenye kuegemea falsafa za kijamaa na uzalendo, aligusia kwa kina kuhusu haja ya Tanzania kuwa na katiba mpya.
Akijadili kwenye mjadala huo, alisema ili siasa ya Tanzania istawi vyema lazima kupatikane katiba mpya akisema katiba iliyopo siyo muafaka kwa Tanzania ya sasa yenye kufuata mfumo wa vyama vingi.
Hata hivyo, msomi huyo ameanza kuchanga upya karata zake akifuata nyayo za wasomi waliomtangulia ambao kwa nyakati tofauti waliachana na ufundishaji katika vyuo vikuu na kujiunga serikalini ama katika taasisi nyingine za kiutendaji.
Huku akitetea nafasi yake ya awali ya uchambuzi, Dk Bashiru amejibu hoja ya waandishi wa habari waliotaka kujua kama ataendelea na msimamo huo au la akisema kuwa, "kazi niliyopewa si ya jukwaa au siasa za majukwaani, siasa za majukwaani ni mwenyekiti wa chama. Na ni marufuku kwa mtendaji kufanya kazi ya mwanasiasa."
Kwaherini. Abdurahman Kinana akiwaaga wana CCM
Kuteuliwa kwake ndani ya CCM kumekuja siku chache baada ya kuongoza kamati iliyoundwa na mwenyekiti Rais John Magufuli iliyokuwa ikichunguza mali ya chama na kisha kuwasilisha ripoti yake ambayo iliwatuhumu baadhi ya vigogo wa chama hicho kuhusika katika kuhujumu mali hizo.
Ama, Dk Bashiru aliyekuwa mkufunzi wa masuala ya siasa na utawala wa umma katika chuo kikuu cha Dar es Salaam sasa anaingia katika orodha ya wasomi wengi ikiwamo maprofesa waliochana na taalamu zao na kuchukua majukumu serikalini.
Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaonyesha wasiwasi kuhusu kuendelea kupukutika kwa wasomi wa ngazi za juu wanaobadili taaluma zao baada ya kukabidhiwa majukumu mengine serikalini.
Moja ya kizingiti ambacho kitakuwa ni mtihani wake wa kwanza ni namna atakavyofanikiwa kushughulikia ubadhirifu alioubaini wakati alipokuwa katika kamati ya kutathmini mali za chama.
Maoni