Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Samwel Opulukwa amesema Serikali itaanzisha Magereza katika wilaya hiyo ili kuwafunga vijana wavivu wasiotaka kufanya kazi.
Mh. Opulukwa ameyasema hayo wakati alipotembelea Miradi mbalimbali ya Maendeleo ikiwemo kilimo, afya na elimu inayotekelezwa na kampuni ya Mgodi ya Shanta Mining katika kata ya Mbangala.
Amesema vijana wengi katika kata hiyo hawapendi kufanya kazi licha ya kuwa na fursa nyingi ikiwemo ardhi yenye rutuba na badala yake wamekuwa wakijiingiza kwenye vitendo vya ulevi.
Kiongozi huyo wa wilaya amemweleza Kamishna Jenerali wa Magereza kuangalia uwezekano wa kujenga Gereza la Wilaya ili kuwafunga vijana ambao hawataki kufanya kazi pamoja na wahalifu wengine.
“Haiwezekani vijana mnashindwa kulima wakati Mashamba yapo,huku kwetu kuna fursa nyingi lakini mnashindwa kuzitumia, pale mkwajuni kulikua kuna kazi na mkandarasi lakini watu wakifanya kazi kidogo wakilipwa wanaingia mitini. Sasa tukiwa na gereza tutawafunga miezi mitatu halafu mnafanya kazi kwa lazima mkiwa ndani nawaambia mtalima tu kwa nguvu mkiwa huko gerezani," amesema.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya ameagiza kila kaya kulima hekari tano za ufuta ili kujiongezea kipato na kuondokana na umasikini.
Maoni