MTEULE THE BEST
Diamond Platnumz: Ni wakati wangu sasa kuwasaidia watanzania
Hapana shaka sanaa zinazoitoa Tanzania kimasomaso kwa sasa ni
muziki wa kizazi kipya, kwa kuwa umekuwa tegemeo pekee la kushinda
katika nafasi mbalimbali wasanii wanazowania ikilinganishwa na fani
nyingine za sanaa na michezo.
Mbali na kuiwakilisha
vema nchi Kimataifa pia muziki huo umekuwa ukichangia pato la Taifa na
kuboresha maisha ya baadhi ya Watanzania.
Msanii kutoka
Tandale, Diamond Platnumz ni miongoni mwa wasanii hao baada ya kufanya
vema kimataifa sasa anarudi nyumbani na kuiambia jamii asante.
Katika
mahojiano yake na Starehe Diamond alisema alianza kuwashukuru wananchi
wa Tandale kwa kuwalipia bima ya afya baadhi yao na kusaidia kutatua
matatizo ya baadhi ya shule.
Alisema ameguswa zaidi na changamoto wanazokutana nazo wanafunzi kutokana na kukumbuka alikotoka.
“Unajua
mimi nimesoma kwa shida, nimekuwa kwa shida, nimeishi kwa shida,
sitamani kuona mtu mwingine akipitia hayo ndiyo maana ninapoweza
kusaidia nafanya hivyo, ” alisema Diamond.
Alisema
ameanza na Jiji la Dar es Salaam kwa sababu ndiko alikokulia na maeneo
yenye mahitaji anayafahamu sasa anajipanga kwenda mikoani.
Alifafanua
kila jambo lina wakati wake, lakini mipango yake ni kuhakikisha kidogo
anachokipata anakipeleka kwa wanafunzi ambao anaamini hawana jinsi zaidi
ya kusoma na hawana wa kuwatetea zaidi ya anayefahamu maisha halisi ya
shule za Kayumba.
Katika kuonyesha amelipania hilo
ameungana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutatua tatizo
la madawati kwa kutumia Sh 48 milioni kutengeneza madawati imara
yatakayodumu kwa miaka mitano kwa ajili ya shule za mkoa huo.
Alisema
Makonda anapambana kuwasaidia wanafunzi wanaosoma katika mazingira kama
aliyosomea yeye, hivyo hana budi kuungana naye katika mapambano hayo.
Diamond
ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa lebo ya muziki (WCB) alisema
kutokana na mkuu wa mkoa huyo kuchukulia sanaa ni moja ya taaluma kama
nyingine wameona ni vema kurudisha faida wanayoipata kwa jamii hasa
anapoona kuna mafanikio katika kazi wanayofanya.
“Tunamshukuru
Paul Makonda kukubali kuwa mlezi wetu WCB, tutahakikisha kila
tunalolifanya tutafanya kwa bidii kwa lengo la kutomuangusha mlezi wetu,
ambaye ameonekana hataki masihara katika kazi.
“Tutahakikisha
tunaendelea kusaidia kundi kubwa la vijana hususani katika sanaa kwa
kuwashika mikono kukuza vipaji vyao,” alisema Diamond.
Makonda alisema msanii huyo amekuwa wa kwanza nchini kuguswa na kufanya jambo la kizalendo la kuunga mkono jitihada za Serikali.
“Namshukuru
Diamond na uongozi wa WCB kwa kuisaidia jamii hususani wadogo zenu
waliopo shuleni, mmeonyesha uzalendo wa hali ya juu kuungana na jitihada
za Rais John Magufuli katika kuhakikisha elimu bure inapatikana na
kuhakikisha changamoto mbalimbali zinamalizika,” alisema.
Atengeneza ajira 43
Licha
ya kufanya vizuri katika kazi zake za muziki, Diamond amefanikiwa
kutengeneza ajira 43 mpaka sasa na anatarajiwa kutengeneza ajira kwa
wasomi kadhaa baada ya kuanzisha kampuni nyingine.
Kujituma
kwa msanii huyu kunaifanya Tanzania kuanza kufikiria upya ni namna gani
inaweza kutumia vipaji katika kutengeneza ajira kwa wasomi
wanaozalishwa kila uchao katika vyuo vikuu mbalimbali na kukosa ajira.
Makonda
alisema licha ya kutoa msaada huo, Diamond ana nafasi ya kuajiri wasomi
na wataalamu mbalimbali kutokana na kuanzisha kampuni hiyo ya WCB
inayojihusisha na masuala mbalimbali ikiwamo kuibua vipaji vipya.
“Diamond
kupitia kampuni yake atahitaji watu wa sheria atakaowatumia wakati wa
kuingia mikataba, wataalamu wa teknolojia watakaosimamia blog, nembo za
kazi zake, watunza fedha kwa ajili ya kusimamia mapato na matumizi,”
alisema Makonda.
Kuhusu WCB
WCB
ni kampuni inayomilikiwa na mwanamuziki Diamond inajishughulisha na
kurekodi video na audio na kusimamia wasanii (record label).
Ndani ya kampuni hiyo iliyoajiri wafanyakazi 43 kuna studio ya kupiga picha .
Kampuni inajihusisha pia na kuandaa matangazo ya biashara.
Kwa
upande wa wasanii waliosaini mkataba la lebo ya kampuni hiyo,
wanasimamiwa katika usambazaji wa kazi zao, utangazaji, kurekodi kazi za
muziki video na audio, huku shughuli za msanii husika ikiwa ni utunzi,
uimbaji na shoo.
Maoni