MTEULE THE BEST
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza amezindua kampeni ya kufanyika kwa kura ya maamuzi ambayo inatazamwa na jaribio la kutaka kusalia madarakani hadi 2034.
Shirika la habari la AFP linasema mpango huo unahusisha kuidhinishwa kwa rasimu ya katiba ambayo itamuwezesha kuwania urais kwa mihula miwili zaidi ya miaka saba kila muhula.
Muhula wa sasa wa Bw Nkurunziza unafikia kikomo 2020.
Rais huyo aliwaambia wafuasi wake Jumanne katika kijiji cha Gitega kwamba wale wanaopinga juhudi zake "kwa maneno au kwa vitendo" watakuwa wameuvuka "mstari mwekundu".
Kampeni hiyo imeanzishwa baada ya serikali kuzindua juhudi za kuchangisha fedha za maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Shirika la habari la AFP linasema mchango huo, ambao serikali inasema ni wa hiari, umeshutumiwa na makundi ya kutetea haki za kibinadamu ambayo yamesema ni kama "wizi kwa mpango".
Viongozi wa upinzani walio uhamishoni wanasema kura hiyo ya maoni itakuwa kama "mazishi" kwa mwafaka wa amani uliotiwa saini mwaka 2000 nchini humo.
Mkataba huo wa amani ulisaidia kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 13 na kusababisha vifo vya watu 300,000.
Burundi ilitumbukia kwenye mzozo mwingine wa kisiasa mwaka 2015 Rais Nkurunziza alipokataa kung'atuka baada ya kumaliza muhula wake na akaamua kuwania tena urais.
Mwaka huo pia kulitekelezwa jaribio la kuipindua serikali ya Bw Nkurunziza ambalo halikufanikiwa.
Mzozo huo ulisababisha mashambulio ya mara kwa mara ambayo yamechangai vifo vya watu karibu 2,000 na wengine maelfu kutoroka makwao na kukimbilia nchi jirani.
Mazungumzo ambayo yamekuwa yakiendelea kati ya serikali na makundi ya upinzani yalisambaratika wiki iliyopita.
Rais wa zamani wa Tanzania Benjamin Mkapa aliyekuwa anafanikisha mazungumzo hayo alisema hakukuwa na "makubaliano yoyote, maazimio yoyote au stakabadhi yoyote ya kuwafungamanisha wadau".
Maoni