Msajili Msaidizi wa vyama vya siasa nchini, Sisty Nyahonza amesema sheria inaruhusu kuchukua mkondo wake kwa Mbunge yoyote atakayezidisha kutumia gharama kubwa katika chaguzi mbalimbali, ambapo amesema gharama ya juu ni milioni 88.
Hayo amesema kupitia kipindi cha East Africa Breakfast cha East Africa Radio kuwa sheria hiyo imeanza mchakato mwaka 2006 na kukamilika 2010, inasema mtu achaguliwe kutokana na uwezo wake wala sio pesa.
Gharama ya kuendesha kampeni za uchaguzi inatokana na ukubwa wa jimbo lenyewe lakini kuna kiwango maalumu ambacho taasisi imekipanga, kiwango cha chini kinaanzia milioni 33 huku kiwango cha juu ni milion 88.
''Kila jimbo lina kiwango chake , kama kiwango ambacho kimepangwa kikipita tunayo nguvu ya kuchunguza namna gani gharama kubwa imetumika ili muhusika achukuliwe hatua.
Alipoulizwa juu ya kujiridhisha kama kweli wagombea wametumia kiasi ambacho kimepangwa na taasisi hiyo amesema wana njia nyingi ikiwemo kushirikiana na Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
''Tuna njia nyingi za kufahamu kama tuna shaka na matumizi ya kuendesha kampeni zimezidi, tunashirikiana na Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa, tuna uwezo wa kufuata ripoti zote ambazo zimefanyika kupitia chama husika pamoja na kutafuta taarifa kwa wasamalia wema''.
Kwa uchaguzi ambao umefanyika mwaka 2015 kiwango cha chama cha siasa kimeruhusiwa kutumia kiasi cha bilion 17 kwa Rais, Wabunge na Madiwani.
Ambapo katika kampeni za Rais sheria inataka atumie shilingi bilioni 6 hadi mwisho wa uchaguzi, wakati madiwani wanaoishi mijini wametengewa milioni 8 huku wale wa vijijini watumie milion 6.
Katika sheria hiyo majimbo 267 ya Tanzania ambapo wabunge wanagombania wanatakiwa watumie kuanzia milioni 33 kiwango cha mwisho milioni 88 kisizidi zaidi ya hapo. Japo kuna majimbo yanaainishwa kabisa ambayo hayatakiwi kuvuka shilingi milioni 33.
Maoni