Ruka hadi kwenye maudhui makuu

WAKESHA KANISANI WIKIMUOMBEA MAREHEMU AFUFUKE

MCHUNGAJI na waumini wa Kanisa la The Evangelistic Assemblies of God (EAGT) mtaa wa Eden 'A' Manispaa ya Sumbawanga, Rukwa, wamekesha wakimuombea marehemu wao afufuke, wakidai alikufa kwa nguvu ya giza.
Elizabeth Lwitiko (30) alifariki dunia juzi saa tatu asubuhi kutokana na matatizo ya uzazi, wakati akijifungua pacha, aliowaacha hai na wametafutiwa mlezi.. Mchungaji Jacob Lwitiko aliongoza waumini wake, kuchukua mwili wa marehemu chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa, Sumbawanga na kuiweka kwenye madhabahu ya kanisa hilo na kufanya maombezi, wakiamini kuwa huenda atafufuka.
Mchungaji Lwitiko ni kaka wa Elizabeth na aliachiwa uongozi wa kanisa hilo na kaka yake, Amos Lwitiko, mwanzilishi na kwa sasa yuko Makambako mkoani Njombe. Mwenyekiti wa Mtaa wa Edeni ā€œAā€ lililopo kanisa hilo, Gerald Mwazembe alikiri kuwepo kwa mkasa huo, uliowashitua wakazi wa jirani kwani ni mara ya kwanza kutokea.
Akisimulia, alisema kuwa Elizabeth alifariki dunia saa tatu asubuhi katika Kituo cha Afya cha Mazwi mjini hapa kutokana na matatizo ya uzazi, ambapo alipungukiwa damu mwilini baada ya kujifungua salama kwa njia ya kawaida watoto pacha ambao wako hai.
ā€œMwili wa marehemu ulihifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa, lakini waombolezaji na mchungaji wa kanisa hilo waliuchukua mwili huo wakiamini alikufa kishirikina na kwamba wakimwombea angeweza kufufuka,ā€ alieleza.
Alisema mwili ulipofikishwa kanisani hapo, uliwekwa madhabahuni na ibada ya maombezi iliyoambatana na nyimbo na midundo ya ngoma, ilifanyika kuanzia saa sita mchana hadi usiku wa manane huku milango ikiwa imefungwa, wakiamini kuwa atafufuka.
ā€œIlipofika usiku wa manane niliwapigia simu Polisi ambapo askari wa kikosi cha doria walifika kanisani hapo, baada ya mazungumzo marefu waliagiza mwili wa marehemu urejeshwe na kuhifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti ili usiharibike,ā€ alieleza.
Aliongeza Polisi walishuhudia mwili wa marehemu ukiwa umewekwa madhabahuni ;huku waumini wakiupapasa, wakiomba afufuke. Baadhi ya waumini wa kanisa hilo, walisema Mchungaji Lwitiko aliwaongoza kwa mara nyingine kuurejesha mwili wa marehemu ili uhifadhiwe chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa mjini hapa huku wakisisitiza kuwa maombezi yaliyofanyika kanisani hapo ni ya imani yao.
Majirani walieleza umati mkubwa ulifurika katika uwanja wa kanisa hilo, baada ya taarifa kuzagaa kuna marehemu anaombewa mwili wake ukiwa madhabahuni, wakiamini atafufuka.
ā€œLakini walioruhusiwa kuingia kanisani kwa maombezi, lazima awe muumini wa kanisa hilo na baada ya kuingia mlango wa kanisa ulikuwa ukifungwa, ā€œ alieleza mmoja wa waumini. Mwandishi wa habari hizi alifika kanisani hapo jana asubuhi na kukuta milango imefungwa ;huku nyimbo zikiendelea kuimbwa kanisani. Baadaye aliambatana na Mwenyekiti Mwazembe na mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten kuingia kanisani kwa mahojiano na mchungaji, lakini ndugu wa marehemu nusura wawapige, wakidai hawakukaribishwa msibani. ā€œKwanza nyie nani... mmekuja kufanya nini hapa ...ondokeni mara moja ....vinginevyo nendeni hospitali mkaulize uzembe walioufanya na kusababisha kifo chake,ā€ alifoka mmoja wa wanandugu akitishia kuwapiga. Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Dk Halfany Haule alisema anafuatilia tukio hilo na atatoa taarifa baadaye. Taarifa kutoka kanisani hapo, zilieleza msiba huo upo Kitongoji cha Bangwe mjini Sumbawanga.


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MAPENZI: Kuna faida na ni muhimu Mpenzi wako kuwa rafiki yako pia

Kuna faida kubwa kwa wapenzi kuwa marafiki KUTOKANA na mila mbalimbali, baadhi ya watu wamekuwa wakiamini kwamba mwanamke ni daraja la pili. Daraja la kwanza na lenye kuthaminiwa ni mwanaume. Yaani mwanamke hana kauli kwa mwanaume. Anakuwa kama mtumwa fulani hivi.  Mwanaume akiongea, basi ni maelekezo kama vile rais wa nchi anavyotoa maelekezo kwa watu walio chini yake. Hakuna wa kupinga. Akisema sitaki kitu fulani kifanyike, basi ni mpaka atakapotoa maelekezo mengine. Vinginevyo, maelekezo ya awali yatabaki kusimama kama sheria.  Wapo baadhi ya wanawake wanaofurahia aina hii ya uhusiano kwa sababu ya mazoea. Kwamba wamekuzwa hivyo, mwanaume ni mwanaume. Huu ni mfumo ambao watu wengi wamekuwa wakiuishi. Kuna ambao wanakubaliana nao, wengine hawakubaliani nao.  Watu wengi sana wamekuwa wakiishi katika malumbano katika mahusiano yao kutokana na mfumo huu wa maisha. Mwanamke hataki kuishi kama mtumwa, mume anakomaa kuonesha uanaume wake. Hakuna anayekubali kushuka,...

Urusi: Vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini havitafua dafu

MTEULE THE BEST Image caption Waziri wa maswala ya kigeni nchini Urusi Sergei Lavrov na mwenzeka wa Marekani Rex Tillerson Waziri wa maswala ya kigeni nchini Urusi Segei Lavrov amemwambia waziri wa ulinzi nchini Marekani Rex Tillerson kwamba kuiwekea vikwazo zaidi Korea Kaskazini hakutafua dafu. Taarifa iliochapishwa na wizara ya kigeni nchini Urusi inasema kuwa wawili hao walizungumza kwa njia ya simu na kushutumu majaribio ya makombora ya hivi karibuni yaliotekelezwa na Pyongyang . Lakini inasema kuwa bwana Lavrov alisisitiza kwamba diplomasia ndio njia ya pekee ya kumaliza wasiwasi katika rasi ya Korea, na kutaka hatua zozote dhidi ya taifa hilo kusitishwa akionya huenda zikasababisha madhara yasiojulikana. Waziri wa ulinzi nchini Marekani amesisitiza kuwa bado kuna fursa ya kidiplomasia katika kukabiliana na Korea Kaskazini. Mapema rais Trump alichapisha ujumbe katika akaunti yake ya Twitter akisema mazungumzo sio suluhisho.

Fuvu la binadamu wa kale liligunduliwa miaka 60 iliyopita nchini Tanzania

Fuvu la binadamu wa kale liligunduliwa miaka 60 iliyopita nchini Tanzania Miaka 60 siku kama ya leo ugunduzi mkubwa ulifanyika katika eneo la Olduvai Gorge, kwenye kreta ya Ngorongoro. Wanaakiolojia Louis na Mary Leakey waligundua fuvu la mtu anayeaminika kuwa ni wa kale zaidi waliyompa jina la Zinjanthropus. Ugunduzi huo uliofanyika saa nne asubuhi Julai 22, 1959 kipindi hicho kwenye eneo la Tanganyika ulikuwa wa vipande zaidi ya 100 ukasaidia katika kutambua asili ya watu wa awali duniani. Kabla ya ugunduzi huo, wanasayansi na wanahistoria walikuwa wakiamini kuwa binadamu wa kale walitokea Uchina baada ya ugunduzi wa mafuvu ya kale baina ya 1923 na 1927 nchini humo ya Homo eractus, ama maarufu kama Peking Man. Mafuvu hayo ya Uchina yalikuwa na umri wa takribani miaka 750,000. Mafuvu ya Olduvai eneo ambalo kwa sasa lipo Tanzania wakati wa ugunduzi wake lilikuwa na umri wa takribani miaka milioni 1.75, na hakuna mabaki ya mtu wa kale zaidi ambayo mpaka sasa yamegundul...