MTEULE THE BEST
Mechi ya kirafiki iliyopangwa kuchezwa leo kati ya Yanga na Polisi Tanzania itachezwa kesho Jumapili Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.
Afisa habari wa Klabu ya Yanga, Dismas Ten amesema awali, mechi hiyo ilipangwa ichezwe hii leo ikiwa ni maalumu kwa kikosi hicho kuangalia nyota wake baada ya kufanya mazoezi.
"Mechi tulipanga tucheze leo lakini tumeahirisha kwani hapo awali tulipanga ichezwe leo Uwanja wa Taifa lakini Uwanja huo nyasi zake zilikatwa na bado hazijaota na kuwa sawa ili ziwe rafiki kwa wachezaji hivyo tutacheza kesho katika Uwanja wa Uhuru, mashabiki wetu tunaomba wajitokeze ili kuangalia kikosi chao ambacho kinajiandaa na mashindano mbalimbali, " amesema.
Yanga inajiandaa na mashindano mbalimbali ikiwemo yale ya Kimataifa ambapo itaanza na St. Louis ya Shelisheli katika Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mbali na michuano hiyo pia, Yanga inajiandaa na michuano ya Kombe la Mapinduzi itakayoanza kutimua vumbi mwishoni mwa mwezi huu Visiwani Zanzibar, michuano ya kombe la Shirikisho Tanzania na ile ya Ligi kuu ya Soka Tanzania Bara
Maoni